Afisa wa polisi wa Kenya auawa Haiti akilinda doria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123150-afisa_wa_polisi_wa_kenya_auawa_haiti_akilinda_doria
Afisa wa polisi wa Kenya aliyepelekwa Haiti chini ya mpango wa Kikosi cha Kimataifa cha Kulinda Usalama Haiti (MSS) amefariki dunia baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye doria.
(last modified 2025-02-24T08:54:46+00:00 )
Feb 24, 2025 08:54 UTC
  • Afisa wa polisi wa Kenya auawa Haiti akilinda doria

Afisa wa polisi wa Kenya aliyepelekwa Haiti chini ya mpango wa Kikosi cha Kimataifa cha Kulinda Usalama Haiti (MSS) amefariki dunia baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye doria.

Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS) imetuma risala za rambirambi kwa familia ya polisi wa Kenya aliyefariki wakati wa operesheni ya usalama nchini Haiti. 

Operesheni hiyo ilikuwa ikitekelezwa na timu ya usalama ya Kikosi cha Kimataifa cha Kulinda Usalama Haiti jana Jumapili wakati timu hiyo iliposhambuliwa na magenge ya wahalifu katika eneo la SÉGUR – SAVIEN na afisa huyo kujeruhiwa.

Kisha afisa huyo alifariki baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kusafirishwa kwa ndege hadi hospitali ya Aspen Level 2 kwa matibabu.

Huyo ni afisa wa kwanza kufariki tangu maafisa wa polisi wa Kenya walipopelekwa kudumisha amani nchini Haiti.

Kupitia kwa msemaji wa polisi Muchiri Nyaga, idara hiyo inasema familia ya afisa huyo imetaarifiwa kuhusiana na kifo chake.

Kenya imetuma zaidi ya maafisa wa polisi 600 kwenda Haiti kama sehemu ya mpango wa Kikosi cha Kimataifa cha Kulinda Usalama Haiti unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, huku mipango ikiwa ni kutuma jumla ya maafisa 1,000.

Kundi la kwanza liliwasili Juni 2024, na vikundi vilivyofuata vimeendelea kuimarisha juhudi za kupambana na ghasia za magenge na kurejesha utulivu kwa kushirikiana na Polisi wa Kitaifa wa Haiti.

Kikosi cha Kimataifa cha Kulinda Usalama Haiti unajumuisha pia maafisa kutoka Jamaica, Bahamas, Belize, Guatemala na El Salvador, na ulitumwa Haiti ili kusaidia kurejesha udhibiti wa Port-au-Prince kutoka kwa magenge yenye silaha nzito na yaliyojipanga kwa ufanisi ambayo yaliteka sehemu kubwa ya mji mkuu.