Shirika la DAWN lataka ICC imchunguze Rais wa Marekani
(last modified Tue, 25 Feb 2025 02:57:09 GMT )
Feb 25, 2025 02:57 UTC
  • Shirika la DAWN lataka ICC imchunguze Rais wa Marekani

Shirika moja lisilo la serikali limeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuanzisha uchunguzi dhidi ya Rais Donald Trump wa Marekani, kutokana na mienendo yake dhidi ya maafisa wa korti hiyo ya kimataifa iliyoko The Hague huko Uholanzi.

Katika ripoti ya kurasa 172 kwa Mwendesha Mashtaka wa ICC, Karim Khan, shirika la 'Demokrasia kwa Ulimwengu wa Kiarabu Sasa' (DAWN) limeeleza kwamba, Rais Trump anaweza kukabiliwa na "dhima ya jinai ya mtu binafsi kwa kuzuia haki chini ya Kifungu cha 70 cha Mkataba wa Roma" kufuatia amri yake ya kiutendaji ya kuwawekea vikwazo maafisa wa ICC, akiwamo Karim Khan, kwa kuwachunguza maafisa wa Israel.

Raed Jarrar, Mkurugenzi wa Utetezi wa DAWN amesema, “Trump si tu kwamba anazuia haki; anajaribu kuteketeza mahakama ili kuzuia mtu yeyote kuwawajibisha wahalifu wa Israel.”  Kadhalika Jarrar amesema pendekezo la Trump la kuwaondoa kwa nguvu wakazi wa Gaza "linafaa pia kuchunguzwa na ICC".

Mataifa na mashirika mbali mbali duniani yameendelea kukosoa uamuzi wa mapema mwezi huu wa Rais wa Marekani, wa kuiwekea vikwazo ICC, yakiitaja kuwa ni hatua isiyo sahihi.

ICC ilitoa waranti dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa Vita, Yoav Gallant

Televishenii ya NBC pia imeripoti kuwa, nchi 79 zikiwemo Canada, Ujerumani, Ufaransa, Afrika Kusini na Mexico zimetangaza katika taarifa yao ya pamoja kwamba hatua ya Trump ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu inavuruga utawala wa sheria wa kimataifa.

Huko nyuma pia, taasisi ya Democracy for the Arab World Now (DAWN) iliitaka ICC kumchunguza aliyekuwa Rais wa Marekani, Joe Biden kwa kuhusika na uhalifu wa kivita wa Israel dhidi ya Gaza.