Ulaya yakabiliwa na fedheha nyingine kutoka Marekani
Ikiwa ni katika mwendelezo wa fedheha dhidi ya Ulaya, Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, amefuta mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika kati yake na Kaja Kallas, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya.
Mkutano kati ya Kallas na Rubio ulipangwa kufanyika tarehe 26 hadi 27 za mwezi Februari. Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa kufutwa mkutano huo kulifanyika ghafla Kallas akiwa tayari mjini Washington, jambo lililoashiria ongezeko la mvutano wa kisiasa kati ya Ulaya na Marekani.
Awali, gazeti la Financial Times lilieleza kuwa msimamo wa timu ya Donald Trump kuhusu Ukraine unamaanisha kujiweka mbali na utawala wa Kyiv pamoja na kupunguza jukumu la Marekani baada ya vita. Gazeti hilo liliandika kuwa "Marekani sasa imekuwa adui wa Ulaya." Maafisa wa Umoja wa Ulaya wameliambia shirika la Associated Press kuwa walishangazwa na uamuzi huo, huku wakisema kuwa Kallas alikumbwa na "mshituko mkubwa" zaidi kwa sababu alikuwa amepanga mazungumzo yake na Rubio siku mbili tu kabla.
Lengo la safari ya Marekani ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya lilikuwa kuzuia kuongezeka kwa mvutano kati ya Ulaya na Marekani. Katika wiki za hivi karibuni, Rais Donald Trump wa Marekani, ameleta vurugu katika ushirikiano kati ya pande mbili za Bahari ya Atlantiki kwa kutishia kutoza ushuru mkubwa wa forodha bidhaa zinazotoka Ulaya, akidai kuwa zinapaswa kulinganishwa na ushuru unaotozwa bidhaa za Marekani.
Pia, tofauti kuhusu jinsi ya kumaliza vita vya Ukraine bila kuishirikisha Ulaya na bila kuzingatia matarajio yake zimeongeza mvutano wa mahusiano. Maafisa waandamizi wa serikali ya Trump wameionya Ulaya kwamba inapaswa kubeba jukumu la kulinda usalama wake yenyewe, ukiwemo wa Ukraine. Kwa sababu hiyo, Marekani imeiacha Umoja wa Ulaya nje ya mazungumzo ya kumaliza vita hivyo haraka kwa kushirikiana na Russia.
Katika mabadiliko ya nadra ya msimamo, Marekani imepiga kura ya kupinga azimio la Umoja wa Ulaya la kulaani uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.
Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya aliyezungumza na jarida la Politico amesema:
"Inaonekana kuwa serikali ya Trump haikosi fursa yoyote ya kupuuza Umoja wa Ulaya. Anaonyesha wazi kuwa Umoja wa Ulaya hauna tena umuhimu wa kisiasa."

Hivi sasa msimamo wa serikali ya Trump uko karibu zaidi na ule wa Russia kuliko wa nchi za Ulaya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitoa taarifa ikisema kuwa Umoja wa Ulaya hauna nafasi katika mazungumzo ya amani ya Ukraine kwa sababu ya msimamo wake wa kivita.
Wakati huo huo, serikali na maafisa wa Umoja wa Ulaya wanajaribu kujibu kwa utulivu hatua za upande mmoja na za udhalilishaji zinacozhukuliwa na serikali ya Trump. Hata hivyo, msimamo huo haujabadili mtazamo wa Marekani kuhusu Ulaya, badala yake Trump ameendelea kuidharau Ulaya kwa kujiamini zaidi na kutekeleza kwa uthabiti sera yake ya Marekani Kwanza.
Kwa kasi kubwa, Trump amevuruga uhusiano wa miaka 70 wa Ulaya na Marekani katika nyanja za siasa, uchumi, usalama na mazingira. Anataka kuunda upya uhusiano huo kwa kutoa kipaumbele kwa maslahi ya Marekani.
Hata hivyo, Umoja wa Ulaya hauwezi kujibu misimamo hasi ya Trump kwa kasi. Ulaya inapendelea majadiliano na mazungumzo ili kushughulikia mabadiliko haya, lakini serikali ya Trump haitoi muda wa mazungumzo, bali inatarajia matakwa yake yafuatwe kikamilifu.
Kuiondoa serikali ya Ukraine na nchi za Ulaya kutoka kwenye mazungumzo ya amani na Russia ni sehemu ya mkakati huo. Nchi za Ulaya, ambazo zimekuwa na uhusiano wa kina wa kisiasa, kiuchumi, kijeshi, na kiusalama na Marekani kwa zaidi ya miaka 70, sasa zinajikuta zikiwa bila uwezo wa kuhimili dhoruba inayovunja uhusiano huo wa kidiplomasia wa pande mbili za Atlantiki.