Njaa, magonjwa yanawatesa wakimbizi wa Rohingya, Trump apunguza misaada
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123380-njaa_magonjwa_yanawatesa_wakimbizi_wa_rohingya_trump_apunguza_misaada
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi amesema kuwa, uamuzi wa utawala wa Trump huko Marekani wa kusitisha bajeti ya misaada ya kigeni utawaweka maelfu ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya nchini Bangladesh, katika njaa na ukosefu mkubwa zaidi wa usalama.
(last modified 2025-03-01T23:02:05+00:00 )
Mar 01, 2025 23:02 UTC
  • Njaa, magonjwa yanawatesa wakimbizi wa Rohingya, Trump apunguza misaada

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi amesema kuwa, uamuzi wa utawala wa Trump huko Marekani wa kusitisha bajeti ya misaada ya kigeni utawaweka maelfu ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya nchini Bangladesh, katika njaa na ukosefu mkubwa zaidi wa usalama.

Bangladesh imepokea zaidi ya Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya na kuwapa hifadhi katika wilaya ya Cox's Bazar ya kusini mashariki mwa nchi hiyo tangu mabudha wenye chuki na Uislamu walipofanya ukatili wa kuchupa mipaka na kuwaua kikatili na halafu kuwafukuza Waislamu katika maeneo yao nchini Myanmar mwaka 2017. 

Jamii ya Waislamu wa Rohingya wanategemea zaidi misaada kutoka nje kwani hawana fursa ya kupata ajira katika kambi kubwa zaidi za wakimbizi duniani na zenye msongamano mkubwa wa watu kupita kiasi.

Marekani ni miongoni mwa nchi zilizokuwa zinatoa misaada kwa wakimbizi wa Rohingya. Hivi sasa lakini baada ya kuingia madarakani Trump huko Marekani, ameamua kusitishwa kwa siku 90 misaada yote ya kigeni ili kuhakikisha kuwa miradi yote inalingana na sera yake ya "Marekani Kwanza."

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi alitembelea kambi inayohifadhi Warohingya huko Cox's Bazar siku ya Ijumaa na baadaye ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa  X kwamba kupunguzwa misaada kunaweza kuwaweka maelfu ya wakimbizi katika hatari ya njaa, magonjwa na ukosefu wa usalama.

Hivi sasa wakimbizi milioni 1.3 Waislamu wa Rohingya wamerundikana ndani ya kambi 33 huko Cox's Bazar kusini mashariki mwa Bangladesh ambazo zinahesabiwa kuwa ni makazi makubwa zaidi ya wakimbizi duniani.