Marekani yaendelea kuteketea kwa moto, sasa ni Carolina
Maelfu ya Wamarekani wametakiwa kuhama kwenye maeneo manane katika majimbo ya Carolina Kaskazini na Carolina Kusini kutokana na kutokea zaidi ya matukio 175 ya moto.
Televisheni ya Sky News ya Marekani imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, maafisa wa Zima Moto huko Carolina Kaskazini na Kusini wanapambana na moto katika zaidi ya maeneo 175. Kwa mujibu wa taarifa, moto huo unaenea kwa kasi katika majimbo hayo mawili kutokana na hali ya hewa kavu na upepo mkali.
Msimu wa kuteketezwa kwa moto maeneo mbalimbali ya majimbo ya Carolina Kaskazini na Kusini kwa kawaida hushika kasi mwishoni mwa majira ya baridi kali na mwanzoni mwa majira ya machipuo yaani katika miezi ya Machi na Aprili.
Kwa mujibu wa gazeti la Newsweek la Marekani, Gavana wa jimbo la Carolina Kusini, Henry McMaster ametangaza hali ya hatari baada ya moto kuteketeza zaidi ya hekta 1,200 za ardhi katika jimbo hilo. Amechukuua hatua hiyo ili kusaidia juhudi za kuudhibiti moto huo na kusema kwamba unaweza kusambaa na kuteketeza hadi hekta nyingine 3,000 kutokana na hali ya hewa ya ukame na upepo mkali.
Hali ya ukame nchini Marekani sasa imeenea kutoka Florida na Georgia hadi Mid-Atlantic na Kaskazini-mashariki huku baada ya maeneo ya Jersey yakiwa na hali mbaya ya ukame ambayo yanatishia kurindima moto na kuangamiza vibaya mazingira asili.
Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Fox kimeonya kwamba mchanganyiko wa unyevunyevu, upepo mkali na uchakavu wa mimea ni mambo ambayo yanaongeza sana hatari ya moto kuenea na kushindwa kudhibitiwa huko Marekani.