Wachezaji Waislamu wa timu ya taifa ya Ufaransa wazuiwa kufunga Ramadhani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i123472-wachezaji_waislamu_wa_timu_ya_taifa_ya_ufaransa_wazuiwa_kufunga_ramadhani
Wachezaji wa soka Waislamu nchini Ufaransa wamepigwa marufuku kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wanapokuwa wakifanya mazoezi na timu ya taifa.
(last modified 2025-03-04T04:07:23+00:00 )
Mar 04, 2025 04:07 UTC
  • Wachezaji Waislamu wa timu ya taifa ya Ufaransa wazuiwa kufunga Ramadhani

Wachezaji wa soka Waislamu nchini Ufaransa wamepigwa marufuku kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wanapokuwa wakifanya mazoezi na timu ya taifa.

Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) limeanzisha marufuku hiyo, hali iliyozua shutuma za ubaguzi na kuleta mgawanyiko ndani ya timu.

Taarifa zinasema shirikisho hilo limewaambia wachezaji wanaofunga suamu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa hawawezi kufunga wakiwa katika kambi ya mazoezi ya Clairefontaine. Badala yake, wanaweza kufidia siku zao za kufunga baada ya kumalizika mechi za kimataifa.

"Marufuku ya hijabu kwa wanawake, na sasa marufuku ya kufunga kwa wachezaji wanaofunga Ramadhani. Ufaransa inaendelea kuwa bingwa wa sera za chuki dhidi ya Waislamu," alisema mwandishi wa habari za michezo wa Kanada, Shireen Ahmed, kupitia mtandao wa X (Twitter).

Wachezaji wengi wa Les Bleus ni wenye asili ya ya Afrika, wakiwemo Ousmane Dembélé, N’Golo Kanté, Elias Guendouzi, Ibrahima Konaté na Ferland Mendy. Mwaka jana, kiungo chipukizi Mahamadou Diawara alijiondoa katika kikosi cha wachezaji wa chini ya miaka 19 kwa kupinga marufuku hiyo, kulingana na taarifa ya ESPN.

Hii si mara ya kwanza kwa FFF kuzua utata. Mwaka jana, marefa waliamriwa wasisimamishe mechi wakati wa magharibi ili wachezaji wanaofunga waweze kufuturu. Hii ilitofautiana na ligi kama Premier League ya Uingereza na Bundesliga ya Ujerumani, ambazo ziliwaruhusu wachezaji kufuturu.

Mbali na marufuku ya kufunga, FFF pia inazuia wachezaji wa kike kuvaa hijabu, hata baada ya FIFA kuondoa marufuku yake yenyewe.

Mashinikizo ya kuchukua hatua dhidi ya ubaguzi huo katika Mwezi wa Ramadhani yamezidi kuongezeka. Podcasti ya "Everything Is Futbol" imewataka wachezaji Waislamu kususia timu ya taifa ya Ufaransa, ikisema: "Utaona jinsi Ufaransa itakavyobadilika haraka mara watakapogundua hawawezi kuwa na timu bora bila ya wachezaji wengi wenye uraia pacha wa Ufaransa na Afrika."