Mwanamke anayechukia Waislamu apatikana na hatia ubadhirifu Ufaransa
(last modified Tue, 01 Apr 2025 02:40:41 GMT )
Apr 01, 2025 02:40 UTC
  • Mwanamke anayechukia Waislamu apatikana na hatia ubadhirifu Ufaransa

Mahakama moja nchini Ufaransa jana Jumatatu ilimpata na hatia ya ubadhirifu, Marine Le Pen, aliyekuwa mgombea urais wa Ufaransa kwa mihula miwili na kiongozi wa chama cha National Rally (RN) chenye chuki dhidi ya Waislamu. Hukumu hiyo itaathiri mustakabali wake wa kisiasa, hasa kugombea katika uchaguzi wa rais wa Ufaransa wa 2027.

Taarifa ya kutiwa hatiani mwanamke huyo mwenye chuki dhidi ya wageni hasa Waislamu imesema: "Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama ya Paris, Le Pen pamoja na washtakiwa wengine katika kesi hii, wanaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela."

Kwa upande wake, Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, wasiwasi mkubwa wa Le Pen kuhusu athari za haraka za uamuzi huo, ni kwamba hata kama atakata rufaa, utamzuia kugombea urais wa Ufaransa mwaka 2027, hali ambayo huko nyuma alikiri kwamba ni sawa na  "kifo chake cha kisiasa."

Shutuma zilizomtia hatiani mwanasiasa huyo mwenye chuki na Waislamu zinasema kwamba Le Pen alikuwa mkuu wa mfumo ambao ulitumia pesa za Bunge la EU kwa faida ya chama chake kati ya 2011 na 2021. Shirika la Associated Press limeripoti kuwa Le Pen alitumia baadhi ya pesa za Umoja wa Ulaya kuwalipa walinzi wake ambao wakati fulani walikuwa walinzi wa baba yake, pamoja na msaidizi wake wa binafsi.

Mwendesha mashtaka ameiomba mahakama  kumuadhibu Le Pen kifungo cha miaka miwili jela na miaka mitano ya kupigwa marufuku kushiriki kwenye shughuli za kisiasa.