Vyombo vya habari: Putin hatetereshwi na mashinikizo ya Marekani
Vyombo vya habari vya Marekani vimefichua kuwa licha ya mapendekezo yaliyotolewa kwa Putin na mjumbe maalumu wa Trump katika masuala ya Asia Magharibi, lakini bado Putin hayuko tayari kuacha msimamo wake kuhusu Ukraine.
Shirika la Habari la Mehr limenukuu habari hiyo na kuandika kuwa, licha ya juhudi za Washington za nyuma ya pazia za kujaribu kuifurahisha Kremlin na kuendeleza makubaliano ya amani kati ya Russia na Ukraine, lakini duru za habari zimeliambia gazeti "The Washington Post" kwamba Rais Vladimir Putin wa Russia hajalegeza msimamo wake kuhusu Ukraine.
Steve Witkoff, mjumbe maalumu wa Trump katika eneo la Asia Magharibi alizungumza na Putin kwa zaidi ya saa nne mwezi huu, akijaribu kuandaa pendekezo ambalo lingekubaliwa na Russia lakini kwa mujibu wa gazeti la Marekani la The Washington Post, Vladimir Putin amekataa kulegeza kamba.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mfumo uliopendekezwa wa Witkoff ulijumuisha makubaliano makubwa ya usalama kwa Moscow, ambayo yamepingwa vikali na Ukraine na washirika wake wa Magharibi.
Kwa upande wake, tovuti ya habari ya Bloomberg imeripoti kuwa, serikali ya Marekani inafikiria kutambua rasmi haki ya Russia ya kuidhibiti Rasi ya Crimea kama sehemu ya makubaliano mapana ya amani kati ya Moscow na Kyiv, lakini uamuzi wa mwisho bado haujafikiwa.
Kwa mujibu wa duru mbalimbali za kuaminika zilizozungumwa na Bloomberg News, Marekani iliwasilisha mapendekezo kadhaa kwa washirika wake mjini Paris siku ya Alkhamisi, ikiwa ni pamoja na masharti ya kusitishwa vita Ukraine, kulegezwa vikwazo dhidi ya Russia iwapo makubaliano yatafikiwa na kurejeshwa utulivu. Hii ina maana kwamba maeneo mengi ya Ukraine yataendelea kuwa chini ya udhibiti wa Russia.