Onyo la Marekani kuhusu kurejea nyuma katika mazungumzo ya vita vya Ukraine
(last modified Mon, 21 Apr 2025 02:24:11 GMT )
Apr 21, 2025 02:24 UTC
  • Marco Rubio
    Marco Rubio

Marco Rubio Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ametangaza kuwa, Rais Donald Trump atajiondoa katika juhudi za kupatanisha makubaliano ya amani kati ya Russia na Ukraine ndani ya siku chache zijazo isipokuwa kama kutakuwa na dalili za wazi kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa.

Rubio amesema baada ya kukutana na viongozi wa Ulaya na Ukraine huko Paris kwamba: Hatutaendelea na juhudi hizi kwa wiki na miezi. Kwa hivyo sasa tunapaswa kuamua haraka sana, ninamaanisha ndani ya siku chache, kama [makubaliano] haya yanaweza kufikiwa katika wiki chache zijazo au la.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani aliongeza kuwa, iwapo makubaliano ya amani kati ya Russia na Ukraine yanawezekana wakati huu, basi "tutasalia humo." Ikiwa sivyo, tuna vipaumbele vingine vya kuzingatia." Alibainisha kuwa Donald Trump bado ana nia ya kuhakikisha makubaliano yanafikiwa, lakini yuko tayari kuondoka ikiwa hakuna dalili za haraka za kupigwa hatua kuhusiana na hilo.

Matamshi mapya ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, ambayo yanaonyesha "kuongezeka kwa kutoridhika na kutopiga hatua juhudi za kutatua orodha inayoongezeka ya changamoto za kijiografia" na kukata tamaa Marekani katika kuanzisha usitishaji mapigano katika vita vya Ukraine yanatolewa wakati Rais wa Marekani mwenye utata Donald Trump alikuwa ameahidi wakati wa kampeni zake za uchaguzi kumaliza vita nchini Ukraine ndani ya saa 24 za kwanza katika Ikulu ya White House.

Baada ya kurejea madarakani alirekebisha dai hili na akapendekeza kufikiwa makubaliano kabla ya Aprili au Mei mwaka huu.

 

Hata hivyo, sasa imedhihirika kuwa vita vya Ukraine vina utata zaidi na mitazamo, utendaji, na maslahi ya Russia na Ukraine na hali ya mambo ni ngumu zaidi kuliko vile Trump alivyofikiria kijuujuu kwamba, angeweza kumaliza vita hivi vilivyoenea na vilivyoleta majanga.

Wakati huo huo, suala hili linaonyesha kupungua kwa ushawishi wa Marekani katika uwanja wa kimataifa kama mpatanishi au nguvu kubwa ambayo haiwezi kumaliza mizozo na migogoro kwa kutumia diplomasia na nguvu laini.

Nukta nyingine ni kwamba, mtazamo wa Washington katika vita vya Ukraine umekuwa mojawapo ya sababu za kuongezeka mpasuko katika mahusiano ya Ulaya na Marekani. Ingawa Marekani imetoa wito wa kusitishwa kwa vita nchini Ukraine wakati wa muhula wa pili wa rais Donald Trump, nchi wanachama wa NATO barani Ulaya hazina mtazamo chanya kuhusu mtazamo wa Trump.

Mabadiliko ya sera ya Washington kuhusu vita nchini Ukraine yamekabiliwa na wasiwasi na ukosoaji mkubwa kutoka kwa watu wa Ulaya. Nchi za Ulaya sasa zina wasiwasi kuhusu mabadiliko makubwa katika mtazamo wa Marekani katika vita vya Ukraine, pamoja na kusitishwa kwa silaha na misaada ya kijeshi ya Washington kwa Kiev. Kufikiwa kwa hili kutapelekea kuongezeka kwa mashinikizo dhidi ya Ulaya kwa ajili ya kufadhili na kusaidia vita vya Ukraine.

Hii imesababisha safari ya ujumbe wa Marekani kwenda Paris. Kuhusiana na hili, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio na mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Steve Witkoff walisafiri hadi Ufaransa kushiriki katika mkutano wa Paris na kufanya mazungumzo na viongozi wa Ulaya na Ukraine kuhusu mustakabali wa Kiev.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyataja mazungumzo hayo kuwa ni hatua muhimu kuelekea mitazamo mimoja, kwani wakati wa mazungumzo haya, Witkoff, kama mpatanishi mkuu wa Trump, alizungumza moja kwa moja na kwa mara ya kwanza na Rais wa Russia Vladimir Putin na maafisa wa Ukraine.

 

Baada ya kuhudhuria mkutano huo, Rubio aliandika katika ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X: "Lengo la Marekani ni kutafuta masuluhisho ya vitendo ili kumaliza vita nchini Ukraine." Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ilitangaza kuhusiana na suala hili kwamba, mpango wa amani wa Trump, ambao uliwasilishwa kwenye mkutano wa Paris, ulikaribishwa na maafisa waliohudhuria mkutano huo. Mazungumzo haya yamepangwa kuendelea wiki ijayo mjini London.

Shirika la Habari la Bloomberg limeripoti kuhusu mpango wa amani wa Trump wa kusuluhisha mzozo wa Ukraine, ambao utapelekea kumalizika kwa vita nchini Ukraine, huku maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukraine yakisalia chini ya udhibiti wa Moscow na azma ya Kiev ya kujiunga na NATO ikiondolewa katika ajenda hiyo. Donald Trump pia alitangaza kuwa anatarajia jibu kutoka kwa Urusi wiki hii kuhusu uwezekano wa kusitishwa kwa mapigano nchini Ukraine.

Pia hakuondoa uwezekano wa kuweka hatua za kiuchumi dhidi ya Russia ikiwa Moscow haitajibu mpango huo wa Marekani. Pamoja na hayo inaonekana ni jambo lililo mbali kwamba Moscow, ambayo sasa iko katika nafasi ya juu zaidi katika vita vya Ukraine, italegeza msimamo wake uliokusudiwa kwa ajili ya kusitisha vita vya Ukraine na amani kati ya Russia na Ukraine, licha ya vitisho vya Trump.