Wapakistan waandamana na kutoa kaulimbiu ya "Labaik Ya Al-Aqswa"
Maandamano makubwa yamefanyika katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad kwa ushiriki mkubwa wa matabaka mbalimbali ya wananchi na kuuunga mkono kadhia ya Palestina.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara na kaulimbiu ya "Labaik Ya Al-Aqswa".
Aidha waandamanaji hao wametangaza mshikamano na watu wanaodhulumiwa wa Gaza na kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni.
Washiriki wa maandamano hayo wameeleza kukerwa na kuchukizwa kwao na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni, na pia wametoa wito wa kukomeshwa ukatili wa Wazayuni na kusitishwa uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni katika mauaji ya Wapalestina.
Mohammad Zamin, mmoja wa washiriki wa maandamano hayo amesema katika mahojiano na ripota wa Al-Alam: "Hatuwezi tena kuvumilia jinai na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Marekani." "Dhulma hii lazima ikome mara moja, na Marekani na Israel lazima zijue kwamba Umma wa Kiislamu sio mwanasesere wao."
Ahmed Khan, mshiriki mwingine katika maandamano hayo, aliashiria jukumu la mashirika ya haki za binadamu na jamii ya kimataifa, na kusema: "Ulimwengu na mashirika ya haki za binadamu yanadai kulinda maisha ya watu wapi sasa hivi?
Madai yao ya uwongo yamethibitishwa kwa kila mtu mbele ya ukubwa wa uhalifu unaofanywa na Israel na Marekani huko Gaza, na kauli mbiu zao za kutetea haki za binadamu ni maonyesho.