Nani anafuatia baada ya Wapalestina kufukuzwa kwao? Wasomi wa Ufaransa watetea uamuzi wa Macron
Kundi la wasomi wa Ufaransa limelaani itikadi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kujiona bora na juu ya kila kitu.
Wasomi hao wa Ufaransa wamechapisha makala katika gazeti la Le Monde wakilaani siasa za misimamo mikali za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuzitaka nchi za Ulaya kupinga mpango wa kuwatimua mamilioni ya Wapalestina katika ardhi na nchi yao.
Wasomi hao wa Ufaransa wamekosoa siasa za serikali ya Benjamin Netanyahu na kutangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel, chini ya ushawishi wa makundi yenye misimamo mikali, unatekeleza mpango wa kutimua mamilioni ya Wapalestina kutoka Gaza na pengine Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Mpango huo, ambao unasimamiwa na shirika jipya la "Taasisi ya Uhamiaji" inayoongozwa na Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, unalenga kuangamiza kizazi cha Wapalestina. Waandishi wanaitambua hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, kanuni za maadili na haki za binadamu, na kuonya kwamba maisha ya mamilioni ya Wapalestina yako hatarini.

Wasomi hao wa Ufaransa wamesema kuwa utawala wa Kizayuni, kwa msaada wa Marekani, unaandaa mazingira ya kufukuzwa Wapalestina milioni mbili katika nchi yao katika mazingira ya kinyama, chini ya mashambulizi ya mabomu na mateso ya njaa. Wamesema, vitendo hivi, vinavyoelezwa kuwa ni mauaji ya halaiki au uhalifu dhidi ya ubinadamu, ni sehemu ya itikadi mpya ya Israel ya kujiona juu na bora zaidi na kutaka kulazimisha matakwa yake bila kujali haki za mataifa mengine.
Wasomi wa Ufaransa wameutambua uamuzi wa Rais Emmanuel Macron wa kuitambua rasmi Palestina mwezi Juni mwaka huu kuwa ni jambo la kutia matumaini, lakini wanasisitiza kuwa bila kuchukuliwa hatua za haraka za kuwaokoa Wapalestina, mpango huo hautafanikiwa.
Wameonya kuwa kukubali sera za itikadi kali za kupindukia mipaka za Israel kunaweza kuwa kigezo cha kuigwa na serikali za nchi nyingine, wakihoji kwamba: "Ikiwa leo Wapalestina watafukuzwa katika nchi yao, kesho itakuwa zamu ya nani?"