The Guardian: Magereza ya Ugiriki yamejaa wakimbizi wa Sudan
(last modified Wed, 30 Apr 2025 07:19:24 GMT )
Apr 30, 2025 07:19 UTC
  • The Guardian: Magereza ya Ugiriki yamejaa wakimbizi wa Sudan

Gazeti la The Guardian limeripoti kuwa mamlaka za Ugiriki zinawashikilia mamia ya wahamiaji hususan kutoka Afrika chini ya sheria kali inayopiga marufuku magendo ya binadamu ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 2014 na kuwaadhibu wanaokiuka sheria hiyo hadi kifungo cha miaka 25 jela.

Gazeti hilo limefichua kuwa Wasudani wanaunda kundi la nne kwa ukubwa la wahajiri nchini Ugiriki, na kupita idadi ya wahamiaji wa mataifa mengine, kama vile Wasyria na Wapalestina.

Limewanukuu maafisa wa Ugiriki wakisema kuwa zaidi ya watu 2,500 wamewasili katika kisiwa cha Crete kutoka Afrika kufikia sasa, mwaka huu pekee. Limeeleza kuwa, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi zinaonyesha kuwa idadi ya waliowasili kisiwani humo iliongezeka zaidi ya mara sita mwaka 2024 ikilinganishwa na 2023.

Gabriela Sanchez, mtafiti wa masuala ya uhamiaji katika Chuo Kikuu cha Georgetown, amekosoa jinsi Ugiriki inavyowatendea watu wanaotafuta hifadhi kutoka Sudan. Ameliambia gazeti la The Guardian kwamba kuwatendea watu waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan kama wahalifu ni kinyume na Itifaki ya Umoja wa Mataifa kuhusu Kutorosha Wahamiaji, ambayo inasema wazi kwamba mhamiaji hawezi kufunguliwa mashtaka kwa kuwezesha kusafirishwa kwake. Amesema mwenendo wa nchi za Umoja wa Ulaya wa kuwafungulia mashtaka vijana wahamiaji kwa tuhuma za utoroshaji watu unakinzana na kanuni za itifaki.

Sudan ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la serikali ya nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, ambaye ni kiongozi wa Sudan, na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wanaoongozwa na  Hamdan Dagalo.