Wabunge 60 wa UK waitaka London ilitambue taifa la Palestina
Kufuatia mpango tata wa Israel wa kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Gaza na kuwapeleka Rafah, takriban wabunge 60 wa Uingereza wameitaka serikali ya London kulitambua rasmi taifa la Palestina.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, karibu Wabunge 60 wa Bunge la Uingereza, wengi wao kutoka mirengo ya wastani na ya kushoto ya Chama cha Leba wamemtumia barua Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, David Lammy wakitaka hatua zichukuliwe mara moja.
Watunga sheria hao wa UK wamesema katika barua hiyo kuwa, "Kwa dharura na wasiwasi mkubwa, tunakuandikia kuhusu tangazo la Israel Katz siku ya Jumatatu, akielezea mipango ya kuwahamisha kwa nguvu raia wote wa Palestina huko Gaza hadi kwenye kambi katika mji ulioharibiwa na vita wa Rafah bila kuwaruhusu kuondoka."
Kadhalika wameitaka serikali ya London kulitambua taifa la Palestina mara moja na kuchukua hatua za kuzuia kutekelezwa kwa mpango huo wa kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina wa Gaza.
Wito huo wa wabunge kadhaa wa Uingereza unakuja huku kukiwa na ongezeko la malalamiko ya kimataifa juu ya kampeni ya mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza, ambapo hali ya kibinadamu na kisheria inazidi kuwa mbaya zaidi.