Kwa nini kizazi kipya cha Wamarekani hakiipendi tena Israel?
Kwa miongo kadhaa, kuiunga mkono Israel nchini Marekani haukuwa tu msimamo wa kisiasa bali pia sehemu ya utambulisho wa taifa kwa raia wengi. Katika duru za kisiasa, vyombo vya habari, na taasisi za elimu ya juu, uaminifu kwa Israel ulionekana kama thamani ya pamoja ya Wamarekani. Lakini hali hiyo sasa imebadilika, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.
Takwimu za kura za maoni, ripoti za wachambuzi na hata mijadala kwenye vyombo vya habari vya Marekani zinaonyesha kuporomoka kwa kasi kwa umashuhuri wa Israel miongoni mwa vijana. Mabadiliko haya si mabadiliko ya juujuu tu ya mitazamo ya kijamii, bali ni ishara ya mwamko wa fikra na kuhoji kwa kina simulizi rasmi ambazo zimekuwepo kwa miongo mingi.
Kulingana na utafiti wa Harvard-Harris wa Desemba 2023, zaidi ya nusu ya vijana Wamarekani wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 wanaamini kuwa suluhisho la mgogoro wa Gaza linapatikana tu kwa kuondolewa utawala wa Israel na kuhakikisha Wapalestina wanapata haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe. Aidha, ripoti ya Pew Research ya Aprili 2024 ilionyesha wazi kuwa ni asilimia 14 tu ya vijana wa miaka 18–29 wanaoonyesha kuunga mkono Israel, huku asilimia 33 wakionesha mshikamano na watu wa Palestina.
Lakini kwa nini mabadiliko haya ya msimamo yamejitokeza kwa kasi kubwa miongoni mwa vijana? Jibu linapatikana katika nyanja nyingi: Vyombo vya habari vya kijamii, mabadiliko ya kijamii na kisiasa na vuguvugu la kimaadili linalochochea mwamko huu mpya.
Kwanza, kuibuka kwa mitandao ya kijamii kama sauti mbadala ya vyombo vya habari kumewawezesha vijana kupata ukweli moja kwa moja, bila kuchujwa au kupindishwa na mitazamo ya kimataifa yenye maslahi. Vijana wa Marekani wa leo wanaona kwa macho yao wenyewe watoto waliouawa, nyumba zilizobomolewa, na vilio vya kina mama wa Kipalestina, bila sensa wala taswira ya kipropaganda.
Ukweli unapowasilishwa kwa uhalisia huu wa moja kwa moja, simulizi za vyombo vikuu vya habari vya Magharibi hupoteza mvuto wake wa zamani. Twitter (X), Instagram, TikTok na YouTube zimekuwa majukwaa ya mapambano ya kimtazamo dhidi ya ubanaji wa taarifa. Sauti ya watu wa Gaza na maeneo mengine yaliyovamiwa na kukaliwa kwa mabavu inasikika moja kwa moja, ikigusa dhamira ya kizazi kipya cha vijana wa Magharibi.
Mwamko huu katika vyombo vya kisasa vya habari umechochea harakati mpya za wanafunzi wa vyuo vikuu kupinga siasa za Kizayuni ndani ya Marekani. Maandamano makubwa, migomo ya wanafunzi na wito wa kusitisha uwekezaji wa vyuo vikuu katika makampuni yanayohusiana na Israel ni dalili za mabadiliko makubwa na ya kudumu katika fikra za vijana.
Kadhalika, mabadiliko ya kisiasa ndani ya Marekani nayo yameharakisha mwelekeo huu. Hata kati ya vijana wa chama cha Republican (ambacho kinajulikana kwa uungaji mkono mkubwa kwa Israel), ni asilimia 28 tu ndio bado wanaendelea kuiunga mkono. Kwa upande wa chama cha Democratic, asilimia 47 ya vijana wamesimama pamoja na wananchi wa Palestina. Hili sio pengo la kisiasa tu, bali pia la kimaadili na kiutambulisho.
Kinachovutia zaidi ni kwamba hali hii haijabanwa ndani ya Marekani pekee. Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama wa Taifa ya Israel (INSS), kati ya Oktoba 2023 na Machi 2024, zaidi ya maandamano 2,000 dhidi ya Israel yaliripotiwa kila mwezi kote duniani. Baada ya Yemen, Marekani ndiyo nchi iliyoshuhudia maandamano makubwa zaidi.
Mjumuiko huu wa misimamo ya kimataifa, hasa kutoka kwa vijana wa Kimarekani, umekuwa tishio kubwa kwa utawala wa Israel. Tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, ambapo msaada wa Marekani (hasa kutoka kwa raia wake) ulikuwa msingi wa kuendelea kubakia Israel, sasa nguzo hiyo imeanza kutikisika. Tunashuhudia kile kinachoweza kuitwa “kuporomoka kimtazamo”, kupotea kwa mvuto wa Israel katika dhamira za vijana wa Magharibi.
Tofauti na zamani, Israel haiwezi tena kujificha nyuma ya propaganda na diplomasia za vyombo vya habari. Kizazi kipya ni cha watu walioamka, walioguswa moja kwa moja na ukweli na waliokataa kuwa washirika wa dhulma. Wamechagua kwa hiari, na kwa msingi wa uelewa, kutokuunga mkono kile kinachoonekana kama ukandamizaji wa wazi wa haki za binadamu za Wapalestina.
Kizazi hiki hakichukii Israel kwa jazba, bali kwa maarifa. Hakishangilii Palestina kwa mihemko, bali kwa uelewa wa wazi wa haki, historia na ukweli usio na kificho.
Ulimwengu unaoamka, hauwezi kurudi nyuma. Israel, kwa sasa, inapoteza nafasi yake si tu kwenye uwanja wa kivita, bali pia kwenye uwanja muhimu zaidi, wa fikra za watu. Na hilo, huenda likawa tishio kubwa zaidi kwa maisha ya baadaye ya taifa hilo kuliko hata changamoto za kijeshi au kidiplomasia.
Na kama vile vyombo vya habari vya zamani vilivyounda simulizi za zamani, mitandao mipya imeandika upya simulizi hizo. Na sauti ya kizazi kipya cha Marekani imesikika kwa uwazi: Israel sio tena kipenzi cha mioyo yao. Kwani nyuma ya pazia la propaganda, ukweli kuhusu uovu wa Israel umejitokeza kwa uwazi zaidi.