UNICEF: Watoto 80,000 wako katika hatari kubwa ya kipindupindu Magharibi na Katikati mwa Afrika
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limeripoti kuwa, takriban watoto 80,000 wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu wakati msimu wa mvua utakapoanza katika maeneo ya Magharibi na Katikati mwa Afrika.
Katika taarifa yake, shirika la UNICEF limeeleza kuwa milipuko inayoendelea nchini kujitokeza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Nigeria imezidisha hatari ya kuenea kipindupindu na hivyo kuongeza tishio la maambukizi ya kuvuka mpaka hadi nchi jirani.
Maafisa wa afya wa Kongo, ambayo imeathiriwa pakubwa katika eneo la Maziwa Makuu, mwezi huu wa Julai walisajili wagonjwa wa kipindupindu zaidi ya 38,000 na vifo 951; huku watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano wakiwa ni asilimia 25.6 ya kesi za ugonjwa huo.
Nchi nyingine zinazokabiliana na kipindupindu ni Chad, Jamhuri ya Kongo, Ghana, Ivory Coast na Togo.
Shirika la UNICEF limeongeza kuwa, jitihada za dharura zinahitajika ili kudhibiti na kuzuia kuenea zaidi ugonjwa wa kipindupindu katika eneo hilo zima.
Gilles Fagninou Mkurugenzi wa UNICEF katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika amesema kuwa mvua kubwa, mafuriko na kiwango kikubwa cha watu kuyahama makazi yao vyote vinachochea hatari ya maambukizi ya kipindupindu na kuweka maisha ya watoto hatarini.”