Watoto zaidi ya 300 wameuawa katika mashambulizi mapya ya Israel Gaza
Mamia ya watoto wa Kipalestina wameuawa shahidi tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanze tena operesheni za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Televisheni ya Al Jazeera ikinukuu takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) imeripoti kuwa, zaidi ya watoto 320 wa Kipalestina wameuawa tangu Israel ianze tena operesheni za kijeshi katika Ukanda wa Gaza mnamo Machi 18.
Jumapili, ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya Idul-Fitri huko Palestina, utawala wa Kizayuni uliwaua shahidi Wapalestina 64 wakiwemo watoto 13.
Wakati huo huo, Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, kila kitu katika Ukanda wa Gaza kinakaribia kumalizika ikiwa ni pamoja na misaada na uhai wa watu.
Nalo Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC) limesema kuwa, limeshtushwa na jinsi utawala wa Kizayuni wa Israel unavyofanya jinai za kutisha huko Ghaza bila ya hofu wala kiwewe.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha tena mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza tokea Machi 18, na kuwauwa kwa umati raia zaidi ya 1,000 wa Kipalestina.
Mashambulizi hayo ya kikatili ambayo pia yameshajeruhi Wapalestina zaidi ya 2,300, yanakiuka makubaliano ya kusimamisha vita Ukanda wa Gaza yaliyofikiwa kati ya utawala huo pandikizi na Harakati ya Muqawama ya Hamas.