EU: Idadi ya wahajiri wanaoingia Italia imeongezeka kwa 12%
Shirika la Umoja wa Ulaya la Frontex linaloshughulikia masuala ya mipaka limesema idadi ya wahajiri wanaoingia nchini Italia imeongezeka kwa asilimia 12.
Shirika hilo limesema kuwa, wahajiri 25,000 waliwasili Italia kupitia Bahari ya Mediterranean, kaskzini mwa Afrika mwezi uliopita wa Julai pekee. Limesema kuwa wahajiri 95,000 waliwasili Italia kati ya Januari na Julai mwaka huu.
Shirika la Umoja wa Ulaya la Frontex linaloshughulikia masuala ya mipaka limeongeza kuwa, aghalabu ya wahajiri hao waliowasili nchini Italia ni raia wa Nigeria na Eritrea.
Mapema mwezi uliopita wa Julai, mabaharia na wapiga mbizi wa Kiitalia walisema wamepata miili 217 ya wahajiri kusini mashariki mwa nchi, yapata kilomita 135 kaskazini mwa Libya, siku chache baada ya Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kusema kuwa, yumkini watu 700 wameaga dunia baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya, kusini mwa Italia.
Idadi ya wahajiri haramu wanaojaribu kukimbilia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean imezidi kuongezeka siku hadi siku. Wahajiri karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku wengine zaidi ya 3,000 wakifariki dunia kwa kuzama baharini.