ICC: Vikwazo vya Marekani vimewaathiri majaji, hatutasalimu amri kwa shinikizo lolote
-
Majaji wa makahama ya ICC
Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Jaji Tomoko Akane, amesema kwamba vikwazo vya Marekani vilivyowekwa dhidi ya maafisa wakuu na majaji wa mahakama hiyo vimeathiri moja kwa moja maisha binafsi ya majaji na maafisa walengwa.
Akane amesisitiza, wakati wa ufunguzi wa vikao vya Baraza Kuu la nchi wanachama huko The Hague, kwamba mahakama hiyo "hakitakubali shinikizo la aina yoyote."
Akane amesema, "Uhuru wetu na kutoegemea upande wowote ni nguzo zisizoweza kujadiliwa. Uaminifu wetu unabaki kwa Mkataba wa Roma na sheria za kimataifa."
Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, uliweka vikwazo kwa Mwanasheria Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Karim Khan, manaibu wake wawili, na majaji sita baada ya mahakama hiyo kutoa hati za kimataifa za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Waziri wa zamani wa Vita, Yoav Gallant, kwa mashtaka ya kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza.
Wakati wa kikao cha ufunguzi, Waziri wa Sheria wa Ufaransa, Gérald Darmanin amesisitiza msimamo "usioyumba" ya Ufaransa wa kushikamana na mahakama hiyo.
Waziri huyo wa Ufaransa amelaani alichosema kuwa ni "hatua zisizokubalika za mabavu" zinazowalenga majaji na wanasheria, akiwemo jaji wa Mfaransa.
Mwezi Februari mwaka huu, nchi 79 ambazo zinaunda karibu theluthi mbili ya wanachama wa mahakama ya ICC, zilitangaza uungaji mkono wao kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kuonya kuhusu hatari ya wahalifu kukwepa adhabu na kudhoofika kwa utawala wa sheria za kimataifa, kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Washington dhidi ya mahakama hiyo.