"Silaha za Marekani zinachochea ugaidi Mashariki ya Kati"
Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Kijani nchini Marekani amesema kuna haja ya kuwekewa vikwazo vya silaha nchi zinazochochea machafuko na ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa, Washington imechangia pakubwa hali ya mchafukoge na harakati za ugaidi katika nchi za eneo hilo.
Jill Stein, mwanasiasa wa Chama cha Kijani amesema Marekani inapaswa kuangalia upya sera zake za Mashariki ya Kati na kwamba 'kuwashambulia kwa mabomu na kuwapiga risasi washukiwa wa ugaidi' kumeshindwa kuzima harakati za kigaidi katika eneo hilo. Ameogeza kuwa, mikakati na kampeni za amani ndizo tu zinazoweza kuzima wimbi la ugaidi na ukosefu wa usalama na amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Februari mwaka huu, uchunguzi wa taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI) ulibainisha kuwa Marekani imeongeza biashara yake ya silaha kwa nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya Kati na kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Saudi Arabia inashika nafasi ya kwanza kwa kununua silaha katika eneo la Mashariki ya Kati huku wanunuaji wengine wakubwa wa silaha duniani wakiwa ni India, China na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa, uvamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia nchini Yemen, umeifanya Saudi Arabia kuwa mnunuzi mkubwa wa silaha katika eneo hili. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa taasisi hiyo Aude Fleurant, Marekani imeuza na kutoa misaada ya silaha kwa nchi zisizopungua 96 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kwa thamani ya mbilioni ya dola.
Mgombea wa urais kwa tiketi ya Green Party amesisitiza kuwa, kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS/Daesh sio tishio la moja kwa moja kwa Marekani na hivyo haelewi ni kwa nini serikali ya Washington inadai kuwa inafanya juhudi kubwa za kulitokomeza.