Uvamizi Dhidi ya Iran na Nyufa Ndani ya Ikulu ya Marekani
-
Makamu wa rais wa Marekani, J.D. Vance
Taarifa mpya imefichua kuwa, makamu wa rais wa Marekani, J.D. Vance, tokea alikuwa na mashaka kuhusu vita dhidi ya Iran na hadi sasa anaendelea kupinga mitazamo ya Rais Trump kuhusu vita hivyo ambavyo viko katika wiki ya tatu sasa vimeigharimu Marekani mabilioni ya dola.
Kwa mujibu wa jarida la Politico kuna taswira tofauti ya hali ilivyo ndani ya serikali ya Donald Trump; serikali ambayo kwa nje inaonekana kuwa na msimamo mmoja kuhusu vita, lakini kwa ndani imeanza kuonyesha dalili za mgawanyiko na wasiwasi.
Jarida hilo linadokeza kuwa, wakati mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yakiendelea, mashaka yamejitokeza hata katika ngazi za juu za utawala wa Trump. Ripoti hiyo inaeleza kuwa J.D. Vance, makamu wa rais wa Marekani, tangu mwanzo wa mijadala ndani ya Ikulu ya Marekani alikuwa na mtazamo wa tahadhari kuhusu hatua ya kijeshi dhidi ya Iran na aliibua maswali mazito kuhusu athari zake.
Politico inasisitiza kuwa Vance alikuwa miongoni mwa sauti katika mikutano ya ndani iliyoonya kuhusu hatari ya kuongezeka kwa mzozo na uwezekano wa Marekani kujikuta imezama katika mgogoro mpana zaidi katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).
Kuchapishwa kwa ripoti hii katika wakati ambao serikali ya Trump inaendeleza mashambulizi yake dhidi ya Iran kumewafanya wachambuzi wengi kuelekeza macho yao kwenye uwezekano wa kuwepo nyufa ndani ya duru ya kufanya maamuzi mjini Washington.
Dalili hizi zimeifanya hoja ya tofauti za mitazamo ndani ya serikali ya Marekani kuhusu mashambulizi hayo kupata uzito zaidi. Katika mazingira haya, kuchunguza makundi ya ndani yanayomzunguka Trump, sababu za mashaka ya baadhi ya wahusika wakuu, pamoja na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na tofauti hizi katika kuendelea kwa mashambulizi ya kijeshi, kumekuwa moja ya mada muhimu katika uchambuzi wa maendeleo ya hivi karibuni.
Ingawa serikali ya Donald Trump kwa nje inajaribu kuonyesha sura ya umoja katika msimamo wake kuhusu mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, kuna sababu kadhaa zinazofanya sehemu ya duru ya madaraka mjini Washington , ikiwemo makamu wa rais , kuanza kuwa na shaka kuhusu kuendelea kwa mkondo huu.
Kwanza kabisa ni hofu ya kupanuka kwa mzozo.
Wachambuzi wengi wa Marekani tangu mwanzo waliamini kuwa shambulio lolote la kijeshi dhidi ya Iran linaweza haraka kuvuka mipaka ya operesheni ndogo na kugeuka kuwa mgogoro mpana wa kikanda; mgogoro ambao unaweza kuwahusisha wahusika wengi wa eneo hilo na hata kuyaweka majeshi na kambi za Marekani katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati katika hatari ya majibu ya kulipiza kisasi , jambo ambalo, kwa mujibu wa wachambuzi, limejitokeza katika wiki za hivi karibuni za vita.
Sababu ya pili ni uzoefu wa kihistoria wa vita virefu vya Marekani katika eneo hilo. Kumbukumbu za vita vya Iraq na Afghanistan bado ziko hai katika siasa za Marekani. Vita hivyo vilianza kwa ahadi za operesheni fupi na za haraka, lakini baadaye vikageuka kuwa migogoro mirefu, ya gharama kubwa na ya kuchosha. Kwa baadhi ya wanasiasa wa mkondo unaojulikana kama “America First”, yaani ‘Marekani Kwanza’, ambao Vance pia anaonekana kuwa karibu nao, kuingia katika mgogoro mpya katika Mashariki ya Kati ni sawa na kurudia mkondo ule ule waliokuwa wameonya dhidi yake kwa miaka mingi. Kwa mtazamo huu, mashambulizi mapya yanaweza kuiingiza Marekani tena katika mzunguko wa vita vya gharama kubwa na visivyo na mwisho.
Sababu ya tatu inahusiana na athari za kisiasa ndani ya Marekani. Vita vya nje mara nyingi hugeuka kuwa suala nyeti katika siasa za ndani, hasa pale malengo yake ya kimkakati yanapokuwa hayajaeleweka wazi kwa umma. Baadhi ya wanasiasa wa chama cha Republican, akiwemo Vance mwenyewe, wana wasiwasi kuwa kuendelea kwa mashambulizi haya kunaweza kuongeza mgawanyiko wa kisiasa ndani ya Marekani na kupunguza uungwaji mkono wa wananchi kwa serikali, hasa wakati ambapo jamii ya Marekani inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kijamii.