Ujerumani yakataa ombi la Marekani la kushiriki vita dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i137412-ujerumani_yakataa_ombi_la_marekani_la_kushiriki_vita_dhidi_ya_iran
Kansela wa Ujerumani, amejibu ombi la Donald Trump la kutaka ushiriki wa Berlin katika operesheni ya kijeshi ya Marekani katika Lango Bahari la Hormuz, na kusema wazi kuwa Ujerumani haitashiriki katika vita dhidi ya Iran.
(last modified 2026-03-17T04:43:04+00:00 )
Mar 17, 2026 04:43 UTC
  • Friedrich Merz
    Friedrich Merz

Kansela wa Ujerumani, amejibu ombi la Donald Trump la kutaka ushiriki wa Berlin katika operesheni ya kijeshi ya Marekani katika Lango Bahari la Hormuz, na kusema wazi kuwa Ujerumani haitashiriki katika vita dhidi ya Iran.

Friedrich Merz amenukuliwa na vyombo vya habari akisema: “Berlin haitashiriki katika vita hivi. Serikali ya Ujerumani ilisema wazi tangu siku ya kwanza, na bado tunasisitiza msimamo huo.”

Ameongeza kuwa eneo la Asia ya Magharibi halipaswi kuzamishwa katika vita vya kudumu vyenye malengo yasiyoeleweka, akisisitiza kwamba mgogoro huo unapaswa kumalizika kupitia mpango ulio wazi na mkakati unaoeleweka wa kuufikia mwisho wake.

Wakati huohuo, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani pia amekataa ombi la Trump kwa nchi za Ulaya kushiriki katika juhudi za kufungua tena Lango Bahari la Hormuz.

Boris Pistorius amesema: “Trump anatarajia nini hasa kutoka kwa meli chache za Ulaya ambacho Jeshi la Wanamaji la Marekani, lenye nguvu kubwa, haliwezi kufanya?”

Ameendelea kusisitiza: “Hii si vita vyetu, na sisi hatukuianzisha.”

Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa pia imetangaza katika taarifa rasmi kwamba manowari za nchi hiyo hazitashiriki katika operesheni yoyote ya mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya habari za kimataifa, Wizara hiyo imeeleza kuwa manowari ya kubeba ndege inayotumia nguvu za nyuklia, Charles de Gaulle, pamoja na kikosi chake cha kivita cha baharini, haitahusika katika hatua zozote za mashambulizi dhidi ya Iran.

Rais wa Marekani hivi karibuni alitoa ombi kwa nchi waitifaki kama vile Ufaransa, Uingereza na Japan kujiunga na vita dhidi ya Iran kwa kutuma meli zao za kivita katika Ghuba ya Uajemi.  Awali Trump alidai kwa kiburi kuwa jeshi la mjini la Marekani linaweza kukabiliana na Iran peke yake lakini sasa inaonekana hilo haliwezekani. Hakuna nchi yoyote iliyokubali mwito wa Trump wa kujiunga na vita ilivyoanzisha dhidi ya Iran kwa kushirikiana na utawala haramu wa Israel, jambo linaloashiria kutengwa mtawala huyo wa Marekani.