Pakistan: Saudia ikabidhi usimamizi wa Hija kwa jamii ya Waislamu
Naibu Spika wa Bunge la Pakistan katika jimbo la Sindh ameitaka serikali ya Saudi Arabia ikabidhi usimamizi wa ibada ya Hija kwa jamii ya Waislamu duniani.
Syeda Shehla Raza amesema kuwa, usimamizi wa ibada ya Hija ni jukumu zito ambalo linatakiwa kusimamiwa na nchi zote za Kiislamu duniani ili kuepusha maafa kama yale yaliyotokea mwaka jana katika mji wa Mina nchini Saudia au matukio mengine machungu kama hayo ambayo yamekuwa yakitokea kila mwaka.
Akiashiria ujumbe wa jana wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kwa Waislamu na mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, Shehla Raza amesema kuwa, kuangaliwa upya usimamizi wa Haramu mbili tukufu ya Makkah na Madina kutasaidia kuboresha usimamizi wa ibada ya Hija kwa kusimamiwa na jamii ya Waislamu wote wa dunia.
Naibu Spika wa Bunge la Pakistan katika jimbo la Sindh amegusia mahudhuria makubwa ya Waislamu katika shughuli ya Arobaini ya kumbukumbu mauaji ya mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein kila mwaka katika mji mtakatifu wa Karbala, Iraq na kusema kuwa, licha ya marasimu hayo kuhudhuriwa na mamilioni ya Waislamu kutoka kila pembe ya dunia zaidi ya wale wanaoshiriki ibada ya Hija, lakini hakushuhudiwi maafa ya aina yoyote kutokana na usimamizi mzuri wa serikali ya Baghdad na kwamba suala hilo linadhihirisha wazi kushindwa Aal-Saudi kuendelea kusimamia ibada hiyo tukufu.
Katika sehemu moja ya ujumbe wake kwa Waislamu na Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameashiria tukio chungu la maafa ya Mina na kuzitaka serikali na mataifa ya Kiislamu kuwawajibisha watawala wa Saudia kutokana na jinai wanazozitenda katika ulimwengu wa Kiislamu.