Chuo Kikuu cha Marekani charuhusu bastola darasani
Chuo Kikuu cha Texas mjini Austin nchini Marekani kimewapa idhini wanachuo kuingia na bastola madarasani.
Vyuo vikuu vya Texas vilikuwa vimepigwa marufuku kuwaruhusu wanafunzi kuingia na bastola darasani lakini sasa wataruhusiwa baada ya wabunge wa Marekani, aghalabu yao wakiwa wa chama cha Republican kupasisha sheria ya kuruhusu mpango huo, ambao utaanza kutekelezwa rasmi Agosti mosi mwaka huu. Hata hivyo, sheria hiyo imepiga marufuku kuingia na bastola hizo kwenye mabweni. Mkuu wa Chuo KIkuu cha Texas Greg Fenves ameghadhibishwa na mpango huo wa kuwaruhusu wanafunzi takriban 50,000 kuingia na bastola darasani na kusisitiza kuwa utekelezaji wa sheria hiyo ndio changamoto kubwa zaidi aliyowahi kukumbana nayo katika historia ya uongozi wake chuoni hapo. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani CDC, watu zaidi ya 33,000 huuawa kila mwaka nchini humo kwa kufyatuliwa risasi, ima kwa bahati mbaya, kwa makusudi au kwa kujiua mtu mwenyewe.