Oct 08, 2016 08:11 UTC
  • UNICEF: Wasichana wanatumia saa milioni 160 zaidi kufanya kazi za nyumbani

Wasichana wenye umri wa kati ya miaka 5 na 14 wanatumia asilimia 40 zaidi ya muda au saa milioni 160 kwa siku kufanya kazi za nyumbani zisizo na malipo kote duniani.

Kazi hizo ni pamoja na kuteka maji na kusenya kuni, ikilinganishwa na wavulana, imesema ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyotolewa, kabla ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike itakayoadhimishwa Jumanne ijayo Oktoba 11.

Ripoti hiyo "Kuimarisha Uwezo wa Takwimu kwa ajili ya Wasichana: Kuorodhesha idadi na kuangalia mbele kwa ajili ya ajenda ya 2030, inajumuisha makadirio ya kwanza ya dunia ya wakati unaotumiwa na wasichana kufanya kazi za nyumbani kama vile kupika, kusafisha, kutunza familia, kuteka maji na kusenya kuni.

Ripoti inaonyesha kwamba, tofauti hiyo huanza mapema na mara nyingi kazi zinazofanywa na mtoto wa kike hazionekani na hazithaminiwi. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Somalia, Burkina Faso na Yemen, huku utafiti ukitaja kuwa wasichana weye umri wa miaka 10 na 14 Kusini mwa Asia, Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini hutumia muda mara mbili kufanya kazi za nyumbani kuliko wavulana.

Image Caption

Mwandishi wa ripoti hiyo Claudia Cappa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) anasema, “Kutofautiana kwa hizi kazi za nyumbani kunaonyesha kwamba jukumu la msingi la mtoto wa kike ni kuwa nyumbani na kufanya kazi hizo. Na hii inawafanya kutojitegemea kiuchumi.”

 Bi Claudia anapendekeza kuwa, “Ni muhimu kwamba sisi tunawekeza kwa wasichana katika uwezo wao na kuhakikisha kwamba wanakua kwa kujiamini na kujihisi kuwa na nguvu katika maisha yao. Na ni muhimu pia kuziimarisha jamii na familia ili kuzipa msaada muhimu wa kuwasaidia wasichana.”

Tags