Rouhani: Utamaduni wa Ashura unaweza kuimarisha uthabiti Asia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema iwapo utamaduni wa kuadhimisha kumbukumbu ya Ashura, siku aliyouawa shahidi Imam Hussein AS, Mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW utafuatwa kwa dhati, usalama na uthabiti utarejea katika bara la Asia na ulimwengu wa Kiislamu.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana baada ya kuwasili katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mehrabad hapa Tehran, baada ya safari yake siku sita ya kuzitembelea nchi za kusini mwa Asia na kuongeza kuwa, Waislamu kote duniani wanafaa kuutumia mwezi huu mtufuku wa Muharram kuliombea uthabiti bara Asia na ulimwengu wa Kiislamu.
Amesema ana matumaini kuwa utamaduni wa kumbukumbu ya Ashura na Imam Hussein AS utaleta maendeleo, utulivu, amani na uthabiti katika ulimwengu wa Kiislamu na vile vile katika bara Asia.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kuhusu mafanikio ya ziara yake ya kuzitembelea nchi za kusini mwa Asia na kusema kuwa, mazungumzo yake na viongozi wa nchi za Thailand, Malaysia na Vietnam yamefungua ukurasa mpya wa mahusiano ya pande mbili, kufuatia makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Akizungumza mjini Bangkok nchini Thailand katika kikao cha pili cha Baraza la Mazungumzo na Ushirikiano wa nchi za Asia, Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema nchi za Asia zinapaswa kufunguliana masoko yao, kuwa na ushirikiano wa kiuchumi, kurekebisha miundo yao ya ndani, kuwa wawazi na kufanya mambo kwa mashauriano katika uga wa kisiasa ili kwa njia hiyo, ziweze kupiga hatua kubwa za kuleta ubora wa maisha kwa watu wao na kunyanyua jina la Asia katika miamala ya kimataifa.