China yakosoa chokochoko za kijeshi za Marekani barani Asia
Waziri wa Ulinzi wa China, Chang Wanquan, amekosoa vikali chokochoko za kijeshi za Marekani katika eneo la bara Asia
Akizungumza katika kikao cha saba cha kila mwaka cha ulinzi cha Xiangshan ameashiria chokochoko za hivi karibuni za jeshi la majini la Marekani karibu na visiwa vya China vilivyoko katika Bahari ya Kusini mwa China. Sambaba na hilo Marekani pia imekamilisha mpango wa kuweka mfumo wa makombora wa THAAD nchini Korea Kusini.
Marekani inadai kuwa hatua zake hizo za kijeshi zinalenga kukabiliana na majaribio ya silaha za nyuklia ya Korea Kaskazini.
China hata hivyo imekataa kukubali kisingizio hicho cha Marekani na kusema, Marekani inalenga kubakia kwa muda mrefu kijeshi katika eneo la Asia. Kuna mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiusalama baina ya Marekani na China barani Asia na hilo hasa hubainika wakati wakuu wa nchi hizo mbili wanapozungumza na vyombo vya habari.
Marekani inadai kuwa ina haki ya usafiri baharini katika Bahari ya Kusini mwa China na kwamba inawalinda waitifaki wake wa Asia huku ikidai kuwa China inaeneza ubabe baharini.
Kwa mtazamo wa China, Marekani inalenga kuongoza kijeshi katika eneo la Asia, kuimarisha uwezo wa waitifaki wake sambamba na kuvuruga usalama wa mataifa mengine yasiyo waitifake wake.
Rais Barack Obama wa Marekani anafuata sera za waliomtangulia za kurejea katika zama za vita baridi kwa kuongeza uingiliaji kijeshi na kiuchumi katika eneo la Asia. Chokochoko hizo za Marekani barani Asia ni jambo ambalo limepelekea China kuingiwa na wasiwasi mkubwa.
Katika kikao cha mwaka huu cha saba cha ulinzi cha Xiangshan mjini Beijing, mada kuu umetajwa kuwa ni kuunda kigezo kipya katika uhusiano wa kimataifa.
Weledi wa mambo wanaonya kuhusu natija mbaya iwapo kutaongezeka malumbano baina ya China na Marekani katika eneo la Bahari ya China Kusini na China Mashariki.
Serikali ya China inaamini kuwa, maji wa Bahari ya China Kusini ni milki yake na hivyo inaweza kufanya inavyotaka kijehsi au kiuchumi katika eneo hilo, na kusema Marekani inawahadaa waitifaki wake inapodai kuwa eneo hilo linazozaniwa na si miliki ya China.
Waziri Mkuu wa zamani wa Australia Robert Hawke ameonya kuwa, iwapo msuguano wa baharini baina ya Marekani na China hautatatuliwa, basi kuna uwezekano wa kuibuka mgogoro mkubwa baina ya Beijing na Washington katika eneo hilo.
Hakuna shaka kuwa katika mzozo baina ya China na Marekani, Russia itasimama na China kwa sababu zilizo wazi za kisiasa na kiusalama.