Bensouda: Hatubabaishwi na nchi za Kiafrika kujiondoa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/world-i18442-bensouda_hatubabaishwi_na_nchi_za_kiafrika_kujiondoa_icc
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC amesema licha ya kuwa mahakama hiyo imepata pigo kufuatia hatua ya nchi tatu za Afrika kuanzisha mchakato wa kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma, lakini hatua hiyo haiwezi kuzuia wala kutatiza sughuli za kila siku za mahakama hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2016 03:57 UTC
  • Bensouda: Hatubabaishwi na nchi za Kiafrika kujiondoa ICC

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC amesema licha ya kuwa mahakama hiyo imepata pigo kufuatia hatua ya nchi tatu za Afrika kuanzisha mchakato wa kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma, lakini hatua hiyo haiwezi kuzuia wala kutatiza sughuli za kila siku za mahakama hiyo.

Fatou Bensouda amesema nchi zote 124 wanachama wa ICC zilijiunga na Mktaba wa Roma kwa hiari na pia zina chaguo la kujiondoa lakini amesisitiza kuwa hilo halimaanisha kuwa mahakama hiyo itasitisha shughuli zake kesho.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC

Nchi za Afrika Kusini, Burundi na Gambia tayari zimeanzisha mchakato wa kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi.

Haya yanaarifiwa siku chache baada ya Sidiki Kaba, Mkuu wa ICC pamoja na Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuonyesha masikitiko yao kufuatia hatua ya nchi hizo kujiondoa kutoka katika mahakama hiyo.

Jengo la Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC mjini Hague, Uholanzi

Nchi kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa kwenye mahakama hiyo kutokana na hatua yake ya kuendelea kuwasakama viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi.

Suala hili linatazamiwa kutawala mazungumzo kati ya Rais wa Sudan Omar al-Bashir na Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye alianza ziara rasmi ya kikazi mjini Khartoum hapo jana.