Maandamano ya kuunga mkono Waislamu Warohingya yafanyika mbele ya White House
Makumi ya watu wa jamii ya wachache nchini Myanmar ya Waislamu wa kabila la Rohingya pamoja na wanaharakati wa kisiasa wameandamana hadi mbele ya Ikulu ya Rais wa Marekani, White House kulalamikia sera za viongozi wa Myanmar za mauaji yaliyoratibiwa dhidi ya Waislamu hao.
Waandamanaji hao walitoa sha'ar mbalimbali wakiitaka Marekani na nchi zingine duniani ziingilie kati kwa kuchukua hatua za kuwashinikiza viongozi wa Myanmar ili wakomeshe mauaji ya halaiki, mateso na ukandamizaji dhidi ya jamii ya wachache ya Waislamu wa kabila la Rohingya wanaoishi katika jimbo la Rakhine magharibi mwa nchi hiyo. Waandamanaji hao aidha wametoa wito wa kupelekwa haraka misaada ya kibinadamu kwa Waislamu waishio katika jimbo la Rakhine.
Hayo yamejiri huku timu ya ujumbe wa kimataifa inayojumuisha maafisa wa Umoja wa Mataifa na baadhi ya maafisa wa kiserikali jana asubuhi ikiwasili mjini Mangdo katika jimbo la Rakhine ambapo mbali na kutembelea baadhi ya maeneo ya raia walifanya mazungumzo na wakaazi wa maeneo hayo kuhusu hali yao nchini Myanmar. Hii ni katika hali ambayo maafisa wa serikali ya Myanmar walikuwa wakijaribu kutoa vitisho kwa Waislamu ili wasieleze ukweli kuhusu masaibu yanayowapata.
Watetezi wa haki za binadamu wameripoti kuwa familia zisizopungua 23,000 za Waislamu zilizolazimika kuhama nyumba zao mwezi Oktoba mwaka jana zimebaki bila ya makaazi. Aidha zaidi ya watu 16,000 wa jamii ya Waislamu wa kabila la Rohingya wamelazimika kuhama mkoa wa Rakhine na nyumba 1,077 zimechomwa moto.../