Waislamu Uingereza waelezea wasiwasi wao baada ya Trump kushinda urais Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19228-waislamu_uingereza_waelezea_wasiwasi_wao_baada_ya_trump_kushinda_urais_marekani
Baraza la Waislamu nchini Uingereza limetangaza kuwa, lina wasiwasi mkubwa kutokana na Donald Trump kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2016 00:05 UTC
  • Waislamu Uingereza waelezea wasiwasi wao baada ya Trump kushinda urais Marekani

Baraza la Waislamu nchini Uingereza limetangaza kuwa, lina wasiwasi mkubwa kutokana na Donald Trump kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais nchini Marekani.

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Uingereza amesema kuwa, kuibuka mshindi Trump katika kiti cha urais mtu ambaye katika kampeni zake za uchaguzi alikuwa akitangaza wazi misimamo yake ya kibaguzi dhidi ya Waislamu na wafuasi wa dini za walio wachache ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa.

Harun Khan amesema kuwa, ana matumaini matamshi na maneno yasiyofaa aliyokuwa akiyatamka Donald Trump atayabadilisha na kuyafanya kuwa maridhiano.

Ikumbukwe kuwa, Trump alinukuliwa katika kampeni zake za uchaguzi miezi kadhaa iliyopita akisema kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani atawapiga marufuku Waislamu kuingia nchini humo.

Mazungumzo ya Donald Trump na Barack Obama katika Ikulu ya White House

Matamshi hayo ya kibaguzi ya Trump yalilaaniwa katika kila pembe ya dunia hususan katika Ulimwengu wa Kiislamu. Hata baadhi ya viongozi wa Ulaya akiwemo David Cameron Waziri Mkuu wa Uingereza waliyalaani matamshi hayo ya kibaguzi ya Donald Trump.

Wakati huo huo, Rais Barack Obama na Rais mteule wa Marekani Donald Trump jana walikutana kwa mara ya kwanza katika ikulu ya nchi hiyo White House na kuzungumzia masuala mbalimbali ukiwemo mchakato wa kukabidhiana madaraka.

Trump anatarajiwa kuapishwa Januari mwaka ujao na hivyo kuchukua rasmi hatamu za uongozi wa Marekani akiwa Rais wa 45 wa nchi hiyo.