Mamia ya nyumba za Waislamu wa Myanmar zachomwa moto
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19369-mamia_ya_nyumba_za_waislamu_wa_myanmar_zachomwa_moto
Mamia ya nyumba za Waislamu wa Myanmar zimechomwa moto magharibi mwa nchi hiyo sambamba na kuendelea ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2016 04:46 UTC
  • Mamia ya nyumba za Waislamu wa Myanmar zachomwa moto

Mamia ya nyumba za Waislamu wa Myanmar zimechomwa moto magharibi mwa nchi hiyo sambamba na kuendelea ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch leo limetoa picha za satalaiti zinazoonyesha nyumba za Waislamu wa Rohingya magharibi mwa Myanmar zikichomwa moto. Mmoja wa maafisa wa shirika hilo katika kitengo cha Asia amesema kuwa, uharibu uliofanywa dhidi ya nyumba za Waislamu hao ni mkubwa kuliko walivyokuwa wakidhania hapo awali.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

Waislamu wa myanmar wakikimbia makazi yao

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.

Jumuiya na asasi za kutetea haki za binadamu ulimwenguni zimekuwa zikilaani vikali hatua ya serikali ya Myanmar ya kuhalalisha ukiukaji wa haki za binadamu za Waislamu kwa kutumia kisingizio cha kuimarisha amani na usalama.