Wahajiri wa Kiafrika wazidi kufa maji wakielekea Ulaya
Makumi ya wahajiri wamefariki dunia na wengine wengi kutoweka baada ya boti yao kuzama katika bahari ya Mediterenia wakielekea barani Ulaya jana Alkhamisi.
Loris De Filippi, Rais wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka nchini Italia amesema boti hiyo ya plastiki ambayo katika hali ya kawaida inafaa kubeba watu 120-130, ilikuwa imebeba abiria wengi kupita kiasi na ndiposa ikazama na kwamba zaidi ya watu 100 wanahofiwa kupoteza maisha katika ajali hiyo. Amesema Jeshi la Baharini la Uingereza limewaokoa manusura 27 wa ajali hiyo, yapata maili 20 pwani ya Libya. Amesema aghalabu ya walionusurika katika ajali hiyo ni raia wa nchi za Magharibi mwa Afrika.
Siku ya Jumatano, wahajiri 240 wengine waliripotiwa kuaga dunia katika bahari ya Mediterenia huku wengine 580 wakiokolewa kutoka kwenye boti zilizofurika wahajiri hao haramu.
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Iosta Ibba amewanukuu watu wapatao 15 walionusurika na kufanikiwa kufika salama Catania katika pwani ya mashariki ya Sicily nchini Italia wakieleza kwamba boti waliyosafiria ilipinduka ikiwa na watu 150 ndani yake.
Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Kimataifa la Uhajiri limesema kuwa idadi ya watu waliofariki katika safari hizo hatari za baharini mwaka huu imepindukia 4,270 kulinganisha na 3,777 katika mwaka uliopita wa 2015.