ICC yachunguza magendo ya wahajiri wa Kiafrika nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20011-icc_yachunguza_magendo_ya_wahajiri_wa_kiafrika_nchini_libya
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeanzisha uchunguzi juu ya biashara haramu ya kuwasafirisha wahajiri wa Kiafrika wanaopelekwa barani Ulaya kupitia usafiri hatari wa baharini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 23, 2016 04:30 UTC
  • ICC yachunguza magendo ya wahajiri wa Kiafrika nchini Libya

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeanzisha uchunguzi juu ya biashara haramu ya kuwasafirisha wahajiri wa Kiafrika wanaopelekwa barani Ulaya kupitia usafiri hatari wa baharini.

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mahakama hiyo imeanzisha uchunguzi ili kubaini iwapo magendo ya wahajiri hao wa Kiafrika wanaopelekwa barani Ulaya, yana uzito sawa na jinai za kivita au la.

Amesema iwapo ushahidi utapatikana, kosa hilo linaweza kuhesabiwa kama jinai dhidi ya binadamu huku akisisitiza kuwa tayari ofisi yake imeanza kupokea ushahidi mbali mbali kuhusu biashara hiyo haramu.

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC amesema mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi yumkini ikaanza kutoa waranti za kukamatwa dhidi ya washukiwa wakuu wa magendo ya binadamu.

Haya yanajiri siku chache baada ya Shirika la Kimataifa la Wahamiaji kutangaza kuwa, matukio ya hivi karibuni ya kuzama boti za wahajiri ambao wengi wao wanatokea nchi za magharibi mwa Afrika pamoja na Libya ambao walikuwa wanakusudia kuelekea nchini Italia, yameifanya idadi ya wahajiri waliopoteza maisha katika Bahari ya Mediterranean kufikia watu elfu nne na 636, kiwango cha maafa ya wahajiri baharini kinachokadiriwa kuwa mara sita mwezi huu wa Novemba ikilinganishwa na mwezi kama huu mwaka jana.

Wahajiri wa Kiafika wakielekea Ulaya

Fatou Bensouda amesisitiza kuwa, licha ya kuwa Libya sio mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, lakini waendesha mashtaka wa mahakama hiyo wataendelea kuchunguza magendo ya binadamu nchini humo.