Wanaharakati na wabunge wa Kiislamu Uholanzi wapinga marufuku ya burqa
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na wabunge wa Kiislamu nchini Uholanzi wamepinga vikali hatua ya Bunge la nchi hiyo kupiga marufuku vazi la stara la niqabu au burqa katika baadhi ya maeneo ya umma.
Wabunge wanaoupinga muswada huo wa sheria ya kupiga marufuku burqa katika baadhi ya maeneo ya umma wakiongozwa na Tunahan Kuzu, wanamtuhumu Waziri Mkuu Mark Rutte kuwa anataka kujijenga kisiasa kwa sheria za aina hiyo zilizo dhidi ya Waislamu. Mbunge huyo amesema, uhuru wa kujieleza unawaruhusu watu kuishi wanavyotaka na kuvaa wanavyotaka popote wawapo.
Muswada huo ambao ulipasishwa Jumanne iliyopita na bunge la Uholanzi na ambao sasa unasubiri baraka za Bunge la Seneti, unapiga marufuku kuvaa burqa katika majengo ya serikali, vituo na vyombo vya usafiri wa umma, katika mashule na hospitali.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, yeyote atakayevaa vazi hilo la stara katika maeneo yaliyotajwa atatozwa faini ya Euro 405 sawa na dola 430 za Marekani.
Serikali ya Uholanzi imedai katika taarifa kuwa, ingawaje kila mtu ana uhuru wa kujieleza, lakini uhuru huo una mipaka haswa watu wanapohitajika kuonana moja kwa moja kwa sababu za kiusalama na utoaji mzuri wa huduma.
Mapema mwezi Oktoba mwaka huu, Bulgaria ilijiunga na baadhi ya nchi za Magharibi zilizopiga marufuku vazi la burqa kama vile Canada, Ubelgiji na Ufaransa, baada ya bunge la nchi hiyo kupasisha sheria inayopiga marufuku vazi hilo linalovaliwa na wanawake Waislamu nchini kote.