Uingereza, Marekani zinawatumia magaidi misaada ya silaha
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20818-uingereza_marekani_zinawatumia_magaidi_misaada_ya_silaha
Marekani na Uingereza zinapanga mikakati mipya kuhusu namna ya kuwafikishia silaha magaidi katika maeneo wanayoyadhibiti ya Aleppo au Halab nchini Syria.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 06, 2016 00:08 UTC
  • Uingereza, Marekani zinawatumia magaidi misaada ya silaha

Marekani na Uingereza zinapanga mikakati mipya kuhusu namna ya kuwafikishia silaha magaidi katika maeneo wanayoyadhibiti ya Aleppo au Halab nchini Syria.

Kwa mujibu wa ripoti ya  gazeti la Guardian, maafisa wa ngazi za juu Uingereza na Marekani wanajadili njia  mbali mbali za kuwafikishia misaada magaidi nchini Syria ikiwa ni pamoja na kuiteremsha misaada hiyo kwa miavuli kutoka angani.

Haya yanajiri katika hali ambayo serikali za London na Washington zina wasiwasi kuwa oparesheni kama hiyo yamkini ikapelekea kuibuka makabiliano ya moja kwa moja baina ya majeshi ya nchi hizo na jeshi la Syria.

Gazeti la Guardian limeongeza kuwa, kwa kuzingatia kuwa katika vita vyake dhidi ya magaidi wa ISIS au Daesh nchini Syria, Russia imeweka mfumo wa kisasa wa ulinzi wa anga,  hivyo kuwepo mfumo huo wa makombora ni changamoto kubwa kwa Uingereza na Marekani.

Russia imekuwa ikituhumiwa na Marekani na Uingereza kuwa inaweka vizingiti katika kutumwa kile nchi hizo zinadai ni misaada ya chakula kwa walio katika mzingiro mjini Aleppo. Lengo la tuhuma hizo ni kupotosha fikra za walimwengu kuhusu uungaji mkono wa kisilaha wa madola hayo ya Magharibi kwa magaidi nchini Syria. Misaada hiyo ya silaha hufikishiwa magaidi nyuma ya pazia la misaada ya kibinadamu.

Magaidi wa ISIS

Katika wiki za hivi karibuni nchini Syria tumeshuhudia kushindwa magaidi na waungaji mkono wao ambao miongoni mwao ni baadhi ya madola ya Magharibi na nchi za Kiarabu. Kwa msingi huo madola hayo hivi sasa yanafanya juu chini kuwanusuru magaidi eneo la Aleppo kwa kuwatumia misaada ya silaha.

Misaada kama hiyo  imekuwa ikitumwa kwa muda mrefu sana  na hata gazeti la As Sharq al Awsat linalomilikiwa na utawala wa Saudia, ambao ni muungaji mkono wa magaidi Syria na katika eneo, limekiri kuhusu suala la kupelekewa magaidi misaada. Hivi karibuni gazeti hilo lilimnukulu Charles Lister Mmarekani mtaalamu wa masuala ya Syria akisema kuwa, katika miezi ya hivi karibuni kundi la waasi wanaojiita Jeshi Huru la Syria wamepokea shehena mbili kubwa za msaada wa silaha kutoka nchi za Magharibi.

Hii ni katika hali ambayo Kanali ya Pili ya Televisheni ya Syria imefichua kuwa shehena hiyo ya silaha iliwafikia magaidi wa ISIS na makundi mengine ya magaidi wakufurishaji wanaofungamana na kundi hilo.

Taasisi ya Utafiti ya Carter ya Marekani pia nayo imekiri waziwazi kuwa, kundi la Jabhatun Nusra, linalofungamana na mtandao wa Al Qaeda, ambalo liko katika orodha ya makundi ya kigaidi duniani, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita limepokea silaha kutoka Marekani chini ya jina la Jeshi Huru la Syria na makundi mengine 23 ya wabeba silaha yanayoipinga serikali ya Rais Assad.

Hakuna shaka kuwa, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya ni wafadhili wakuu wa kijeshi na kisilaha kwa makundi ya kigaidi likiwemo ISIS au Daesh.

Haya yanajiri wakati ambao wakuu wa Umoja wa Mataifa wanasisitiza kuhusu ulazima wa kuwekewa vikwazo vya silaha ISIS na kufikishwa kizimbani vinara wa kundi hilo. Pamoja na kuwepo wito huo wa Umoja wa Mataifa, madola ya Magharibi na waitifaki wao katika eneo wanaendelea kuwapa magaidi silaha kwa kisingizio cha misaada ya kibinadamu!

Silaha walizopokonywa magaidi Syria

Kwa kuzingatia ukweli huu, viongozi wa Syria wanasisitiza kuendeleza jitihada zao katika uga wa kuwatumia misaada ya kibinadamu Wasyria sambamba na kutahadharisha kuhusu baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutumia vibaya mgogro wa kibinadamu nchini kwa lengo la kufikia malengo yao ya kuingilia kijeshi nchini humo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio 2170 kuhusu kupokonywa silaha na kusambaratishwa makundi yanayofungamana na Al Qaeda na ISIS. Katika fremu ya azimio hilo, vikwazo vinapaswa kuwekewa wale wote wanaowatumia magaidi misaada ya kifedha au kijeshi. Pamoja na hayo tunaona baadhi ya nchi za Magharibi na hasa Marekani zikidhoofisha azimio hilo kwa vitendo vyao vya kuwapa himaya magaidi.