Wamarekani walio wengi wakiri kwamba, Waislamu wa nchi hiyo wanabaguliwa
Utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa, Wamarekani walio wengi wanaamini kuwa, Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakikabiliwa na vitendo vya ubaguzi nchini humo.
Kituo kimoja cha utafiti nchini Marekani kimetangaza kuwa, wananchi wengi wa nchi hiyo wanaamini kuwa, Waislamu wamekuwa wakibaguliwa nchini humo. Takwimu mpya zilizotolewa na kituo hicho zinaonyesha kuwa, asilimia 82 ya wananchi wa Marekani wanaamini kwamba, Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamwa na vitendo vya dhulma na ubaguzi.
Utafiti huo unasisitiza kwamba, akthari ya viongozi wa harakati za kupigania haki za kiraia wamelaani vikali matamshi ya kibaguzi ya Donald Trump dhidi ya Waislamu aliyoyatoa katika kampeni za uchaguzi.
Katika upande mwingine vyombo vya habari vya Marekani navyo vimekuwa vikieneza propaganda na hisia za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na kufanya njama za kuonyesha kuwa dini hiyo tukufu haina tofauti na misimamo ya kuchupa mipaka.
Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni Wajumbe 291 wa Baraza la Uhusiano wa Kiislamu la Marekani, Maimamu wa Swala za Jamaa, wahadhiri wa Vyuo Vikuu, wanaharakati na viongozi wa jumuiya za Kiislamu wamemuandikia barua ya wazi Rais mteule Donald Trump wakimtaka yeye na baraza lake lijalo la mawaziri kuheshimu sheria za Marekani hususan Katiba ya nchi hiyo.