Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu waanza Tehran
Mkutano wa Kimataifa wa 30 wa Umoja kati ya Waislamu umeanza mapema leo mjini Tehran kwa kaulimbiu ya udharura wa kupambana na makundi ya kitakfiri.
Mkutano huo ambao umefunguliwa rasmi na Rais Hassan Rouhani unahudhuriwa na maulama, wasomi na wanafikra wa Kiislamu zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali za dunia na utaendelea kwa kipindi cha siku tatu.
Mkutano huo wa kimataifa utakuwa na vikao 10 vya kitaalamu ikiwa ni pamoja na kamisheni zinazojadili suala la kupambana na changamoto zinazoukabili Umma wa Kiislamu, hali ya wafuasi wa dini za wachache, umoja wa maulamaa wa muqawama, vyombo vya habari, na kamisheni inayohusiana na masuala ya wanawake.
Sambamba na Mkutano huo wa Umoja wa Kiislamu, kunafanyika tamasha la kwanza la kimataifa la filamu na umoja wa Kiislamu likishirikisha filamu kutoka nchi 37 zinazohusiana na masuala ya ulimwengu wa Kiislamu, shakhsia ya Mtume Muhammad (saw), Qur'ani tukufu, umoja kati ya Waislamu, na vita na propaganda chafu zinazofanywa dhidi ya Uislamu.
Habari kamili kuhusu ufunguzi wa mkutano huo na hotuba ya Rais Hassan Rouhani itakujieni katika matangazo yetu yajayo.