Rais wa Russia awataka walimwengu wapambane kwa dhati na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21847-rais_wa_russia_awataka_walimwengu_wapambane_kwa_dhati_na_ugaidi
Rais Vadimir Putin wa Russia ametoa wito wa kuweko vita vya kweli vya kupambana na ugaidi wa kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2016 03:32 UTC
  • Rais wa Russia awataka walimwengu wapambane kwa dhati na ugaidi

Rais Vadimir Putin wa Russia ametoa wito wa kuweko vita vya kweli vya kupambana na ugaidi wa kimataifa.

Rais wa Russia ameashiria kuenea mashambulio ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ulimwenguni na kuwataka walimwengu wachukue hatua za dhati na za kweli katika kupambana na hujuma hizo za kigaidi ambazo zinatishia usalama wa dunia.

Rais Putin amesisitiza kwamba, ili kuutokomeza ugaidi duniani kuna haja ya kuweko hatua za kweli na dhati za kupambana nao. Rais Putin ameashiria kuuawa kwa kumiminiwa risasi kadhaa balozi wa Russia mjini Ankara Uturuki na kusema kwamba, matukio kama hayo machungu yamekuwa yakitokea katika akthari ya nchi za Ulaya na yanazidi kuongezeka siku baada ya siku.

Andrey Karlov, aliyekuwa balozi wa Russia nchini Uturuki ambaye aliuawa kwa kumiminiwa risasi hiyo juzi

Rais wa Russia amevitaka vikosi vya usalama ndani na nje ya Russia viimarishe usalama na ulinzi kwa ajili ya wanadiplomasia wa nchi hiyo.

Aidha amewataka maafisa wa mashirika ya kijasusi ya siri ya nchi hiyo wawe na ushirikiano zaidi na vyombo vya usalama vya nchi nyingine.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, balozi wa nchi hiyo huko Uturuki ameuawa ili kuvuruga mapambano dhidi ya ugaidi nchini Syria. Akizungumzia tukio la kuuliwa kwa Andrey Karlov aliyekuwa balozi wa Russia nchini Uturuki, Sergei Lavrov amesema kuwa, wahusika wa jinai hiyyo hawawezi kufikia malengo yao.