Guterres: Mgogoro wa Syria ni saratani ya kimataifa
Katibu Mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mgogoro wa Syria umegeuka na kuwa 'saratani ya kimataifa.'
Akizungumza Jumatano katika mahojiano na Televisheni ya SIC ya Ureno, Guterres ameelezea matumaini yake kuwa Marekani na Russia zitaweza kusuluhisha tafauti zao kuhusu namna ya kutatua mgogoro wa Syria.
Marekani na waitifake wake wanaunga mkono uasi dhidi ya serikali ya Syria huku Russia ikimuunga mkono kikamilifu Rais wa Syria Bashar al Assad.
Guterres ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa Ureno amesema mgogoro wa Syria si tu kuwa umepelekea Wasyria kukumbwa na masaibu bali pia ni chanzo cha ugaidi katika maeneo mengine duniani.
Amesema vita vya Syria ni tishio kwa dunia na haviwezi kumalizika hadi pale jamii ya kimataifa itakapotafuta njia muafaka ya kusuluhisha mgogoro katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Wakati huo huo, Russia na Uturuki zinaripotiwa kuafikiana kuhusu mpango wa usutiswahji vita kitaifa baina ya serikali ya Syria na wapinzani wanaobeba silaha. Hayo yamedokezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu ambaye ameongeza kuwa, kuna mapendekezo mawili ya utatuzi wa mgogoro wa Syria ambayo yanajumuisha suluhisho la kisiasa na usitishwaji vita.
Mgogoro wa Syria ulianza Machi mwaka 2011 ambapo magaidi na wanamgambo wanaopata himaya ya kigeni wamekuwa wakiendesha kampeni ya kikatili ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Assad. Syria inazilaumu nchi za Magharibi na waitifaki wao katika eneo kuwa ndio waungaji mkono wakubwa wa ugaidi nchini humo.