Kuendelea mjadala wa kisiasa nchini Marekani kuhusiana na Russia
Suala la kuwepo uwezekano wa kuhusika Russia katika udukuzi wa matokeo ya uchaguzi wa rais uliomalizika hivi karibuni nchini Marekani umeibua mjadapa mkubwa wa kisiasa nchini humo.
Katika hali ambayo Donald Trump, rais mteule wa Marekani pamoja na washauri wake amekataa kuzungumzia kwa kina suala hilo, serikali ya sasa ya Democrat ambayo inakaribia kukabidhi madaraka, vyombo vya intelejensia na hata baadhi ya Warepublican wameendelea kusisitiza juu ya kuhusika serikali ya Moscow katika ushindi wa mfanyabiashara huyo mashuhuri wa Marekani.
Imepangwa kuwa bunge la seneti la nchi hiyo litafanya kikao cha kusikiliza na kuchunguza madai ya hujuma ya udukuzi wa Russia nchini Marekani kwa lengo la kuathiri mwenendo wa matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni. Kuhusu suala hilo, Seneta John McCain wa chama cha Republican na kiongozi wa tume ya huduma za kijeshi ya bunge la seneti la Marekani ametaja hatua hiyo ya Russia kuwa ni kuitangazia vita nchi yake. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya ripoti zinaeleza kwamba Donald Trump amechukua uamuzi wa kuvifanyia marekebisho vyombo vya upelelezi vya Marekani na kupunguza uwezo wa mkuu wa vyombo hivyo.
Kwa sasa na kabla ya kuanza muhula wa uongozi wa rais huyo mteule, ambao utaanza siku 15 zijazo, suala la namna ya kuamiliana na Russia, limegeuka na kuwa moja ya changamoto kubwa kwa serikali ijayo ya rais huyo. Suala hilo halihusiani tu na kadhia ya siasa baina ya Moscow na Washington, bali limegeuka na kutilia shaka uhalali wa kisiasa wa Donald Trump. Sehemu kubwa ya jamii ya Wamarekani miongoni mwa viongozi wa kisiasa wa chama cha Democrat na baadhi kutoka chama cha Republican wamekuwa wakitilia shaka na kujadili kwa kina nafasi ya Rais Vladmir Putin wa Russia katika kuainisha rais wa Marekani. Taasisi tofauti za intelejensia na usalama nchini Marekani zimekuwa zikihusika katika kueneza tetesi hizo.
Hata hivyo ni suala lisilotarajiwa kwa rais ajaye wa nchi hiyo kuafiki kufanyika uchunguzi kuhusiana na nafasi ya Russia kuhusika katika uchaguzi uliopita, kwani suala hilo litatilia shaka uhalali wake wa kisiasa. Pamoja na hayo inatazamiwa kwamba serikali ijayo ya Marekani itakabiliwa na changamoto kubwa katika ushirikiano wake na taasisi kubwa za nchi hiyo kama vile Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) Ofisi Kuu ya Upelelezi wa Polisi (FBI), Shirika la Usalama wa Taifa (NSE) na hatimaye Idara ya Taifa ya Intelijensia. Suala hilo linaweza kuisababishia Marekani madhara makubwa katika kukabiliana na vitisho vya kiupepelezi na kiusalama ndani na nje ya nchi hiyo. Kwa upande mwingine sanjari na kuongezeka tofauti kuhusiana na Russia ndani ya Kongresi ya Marekani, suala la ushirikiano wa karibu baina ya Donald Trump na Rais Vldmir Putin, limewazidishia hasira wanachama wa Republican hususan wahafidhina wa sasa wa chama hicho. Hii ni katika hali ambayo katika kuvutia uungaji mkono, wa bunge la Seneti kwa serikali yake, Trump anahitaji kutekeleza ahadi zake alizozitoa katika kipindi cha kampeni hususan ahadi ya kuondoa bima ya matibabu kwa gharama ya chini maarufu kwa jina la Obama Care na kurekebisha sheria ya ushuru, uhajiri na makumi ya changamoto nyingine. Hii ni katika hali ambayo huku zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kuanza uongozi wa rais huyo mteule, baadhi ya viongozi wa chama chake cha Republican kama vile John McCain, wamesimama kukabiliana na rais huyo mtarajiwa, suala ambalo litapigilia msumari wa matatizo katika uongozi wa Trump.