Obama arefusha hali ya hatari kuhusu Iran
Rais anayeondoka wa Marekani Barak Obama ametia saini sheria ya kuendelezwa sheria ya kitaifa ya hali ya hatari dhidi ya Iran.
Katika barua aliyoandikia Bunge la Kongresi Ijumaa, Obama amesema hali ya hatari dhidi ya Iran iliyotangawzwa Machi 15 1995 itaendelea kuwepo baada ya Machi 15, 2017.
Kwa mujibu wa Sheria ya Hali ya Hatari ya Kitaifa, rais anapaswa kuongeza hali ya hatari ya kitaifa siku 90 kabla ya kumalizika muda wake. Sheria hiyo ya hali ya hatari inampa rais wa Marekani nguvu maalumu ikiwa ni pamoja na kuchukua udhibiti wa mali za nchi husika na pia ni msingi wa vikwazo dhidi ya nchi zinazolengwa. Nchi zingine ambazo Obama amerefusha vikwazo dhidi yao ni Libya, Ukraine, Zimbabwe, Cuba na Venezuela.
Katika barua yake hiyo, Obama alikiri kuwa Iran imetekeleza ahadi zake kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA ambao ulitiwa saini baina ya Iran na madola sita makubwa duniani yaani, China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani mnampo Julai, 14 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 2016.
Obama anatia saini sheria hiyo wiki kadhaa baada ya Baraza la Seneti la Marekani kupitisha muswada wa kurefusha kwa muda wa miaka 10 mingine Sheria ya Vikwazo Dhidi ya Iran (ISA).
Obama hakusaini muswada huo lakini aliruhusu uwe sheria bila ya kuutia saini.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni sawa na kuweka vikwazo vipya na kwamba huo ni ukiukaji wa makubliano ya nyuklia JCPOA yaliyoidhinishwa na jamii ya kimataifa.