Kukiri serikali ya Uingereza juu ya kuweko ubaguzi dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23698-kukiri_serikali_ya_uingereza_juu_ya_kuweko_ubaguzi_dhidi_ya_waislamu
Serikali ya Uingereza imekiri kwamba, Waislamu wa nchi hiyo wanaotafuta kazi wamekuwa wakibaguliwa na kufanyiwa vitendo visivyo vya kiadilifu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2017 23:32 UTC
  • Kukiri serikali ya Uingereza juu ya kuweko ubaguzi dhidi ya Waislamu

Serikali ya Uingereza imekiri kwamba, Waislamu wa nchi hiyo wanaotafuta kazi wamekuwa wakibaguliwa na kufanyiwa vitendo visivyo vya kiadilifu.

Ofisi ya Usawa katika serikali ya Uingereza imetoa taarifa rasmi ikitangaza kuwa, kuna haja ya kufanyika juhudi za kuongeza ufahamu wa waajiri kuhusiana na suala la ubaguzi miongoni mwa Waislamu wanaotafuta kazi. Imeelezwa katika ripoti hiyo kwamba, takribani Waislamu milioni tatu wa Uingereza  wamepitia tajiriba ya kiwango cha juu kabisa cha ubaguzi wakati wa kutafuta kazi na kwamba, mishahara yao ni midogo ikilinganishwa na ya Waingereza wengine ambao ni Wakristo.

Chuki dhidi ya Waislamu

Ubaguzi dhidi ya Waislamu nchini Uingereza na barani Ulaya kwa ujumla hauishii tu katika mambo makhsusi bali wigo wake ni mpana mno. Ubaguzi huo hauishii katika masuala ya kijamii, kiutamaduni na kisiasa tu, bali unaonekana pia hata katika masuala ya kiuchumi na katika kutafuta ajira. Kimsingi ni kuwa, kuenea chuki dhidi ya Uislamu katika madola ya Magharibi ikiwemo Uingereza kumepelekea jamii ya Waislamu izidi kukabiliwa na mbinyo.

Kama ilivyobainisha katika ripoti ya Kamati Teule ya Wanawake na Usawa Katika Bunge la Uingereza mwaka 2016 ni kuwa, Waislamu katika mazingira ya kazi nchini Uingereza hususan katika suala la mishahara na marupurupu wamekuwa wakikabiliwa na ubaguzi mkubwa.

Msikiti mjini Brussels Ubelgiji

Wakati huo huo, kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza kwa sasa limegeuka na kuwa tatizo kubwa la kijamii na kiutamaduni kwa Waislamu wa nchi hiyo ya bara Ulaya. Fauka ya hayo, ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa hujuma na mashambulio ya kibaguzi dhidi ya Waislamu wa Uingereza yameongezeka baada ya wananchi wa nchi hiyo kupiga kura ya kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Aidha chuki dhidi ya Uislamu au kuionesha dini ya Kiislamu kuwa ni tishio pamoja na hatua zilizo dhidi ya Waislamu limegeuka na kuwa tatizo kubwa kwa Waislamu wanaoishi barani Ulaya.

Licha ya kuweko matamshi ya baadhi ya viongozi wa Ulaya eti ya kukabiliana na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na hata kutolewa madai ya kuwaunga mkono Waislamu wa nchi hizo, lakini katika uwanja wa kivitendo tunashuhudia kuongezeka hatua mbalimbali za kuwabana Waislamu katika akthari ya nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Kuendelea mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na kukithiri vitendo vilivyo dhidi ya Waislamu kumezidisha ukosoaji wa asasi za kutetea haki za binadamu, ikiwemo Kamati ya Kupambana na Ubaguzi ya Umoja wa Mataifa.

Ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani

Chuki dhidi ya Uislamu katika madola makubwa barani Ulaya zimekuwa zikifanyika kwa namna mbalimbali kama vile kuwabambikizia kesi Waislamu, kuyavunjia heshima matukufu ya dini yao, propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu sambamba na kutekelezwa ubaguzi wa kila namna katika uga wa kijamii, kiuchumi na hata katika suala la ajira dhidi ya Waislamu. Mfano wa wazi wa jambo hilo ni waajiri kukataa kuwapatia kazi Waislamu au kuwawekea masharti magumu kama vile kuwazuia wanawake wa Kiislamu kuvaa vazi tukufu la hijabu wakiwa makazini.

Hivi sasa kuibuka wimbi la wahajiri wanaoelekea Ulaya ambapo wengi wao ni Waislamu, kumeibua mlolongo wa chuki dhidi ya wahamiaji, dhidi ya wageni na hatimaye dhidi ya Uislamu na kupinga suala la Waislamu kuingia barani Ulaya, masuala ambayo kimsingi yameongeza chuki dhidi ya Waislamu. Mambo hayo ndio yaliyopelekea kushadidi mashinikizo dhidi ya Waislamu wote wanaoishi katika nchi hizo hata kwa wale ambao wanahesabiwa kuwa ni kizazi cha tatu.

Wafuasi wa Begida, moja ya makundi ya kibaguzi nchini Ujerumani

Propaganda chafu za makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali kama ya Pegida nchini Ujerumani, chama cha National Front cha Ufaransa na British Freedom Party cha Uingereza zimekuwa na taathira mbaya katika kushadidisha chuki dhidi ya Uislamu na kuchukuliwa hatua za kuwabana zaidi wafuasi wa dini hiyo tukufu.

Kwa sasa hakuna mwanga na mustakabali mwema wa kubadilika hali hiyo bali mashinikizo dhidi ya Waislamu yameongezeka mno hasa baada ya kutokea hujuma na mashambulio ya kigaidi katika baadhi ya nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa.