Umoja wa Mataifa wampongeza Rais mpya wa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24953-umoja_wa_mataifa_wampongeza_rais_mpya_wa_somalia
Antonio Guterres, Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa amempongeza Rais mpya wa Somalia na kumtaka aunde baraza la mawaziri jumuishi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2017 04:44 UTC
  • Umoja wa Mataifa wampongeza Rais mpya wa Somalia

Antonio Guterres, Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa amempongeza Rais mpya wa Somalia na kumtaka aunde baraza la mawaziri jumuishi.

Guterres kupitia msemaji wake Stephane Dujarric, amesema kipaumbele cha kwanza kwa serikali mpya ya Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo aliyechaguliwa Jumatano iliyopita, ni kukabiliana na baa la njaa lililosababishwa na kiangazi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

kadhalika Katibu Mkuu wa UN ameitaka serikali mpya ya Mogadishu kuharakisha mchakato wa kuundwa kwa katiba na vyombo vya usalama wa taifa vyenye nguvu. 

Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo

Wakati huohuo, Guterres amewapongeza aliyekuwa Hassan Sheikh Mohamud  na Waziri Mkuu wa zamani Omar Abdirashid Ali Sharmarke kwa kushirikiana na rais mpya kuhakikisha kuwa kuna makabidhiano ya amani ya madaraka katika nchi hiyo.

Kauli ya Katibu Mkuu wa UN imetolewa masaa machache baada ya Francisco Caetano, Mjumbe Maalumu wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Afrika na Michael Keating, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia kwa nyakati tofauti kumpongeza Rais Farmajo na kutangaza uungaji mkono wao kwa serikali yake.

Mohamed Abdullahi Farmajo alishinda uchaguzi huo wa Jumatano baada ya Hassan Sheikh Mohamud aliyekuwa akitetea kiti hicho kukubali kushindwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Somalia uliowashirikisha wabunge.