Makundi yaliyo dhidi ya Waislamu yaongezeka kwa kasi Marekani
Idadi ya makundi yaliyo dhidi ya Waislamu yameongezeka karibu mara tatu Marekani mwaka 2016 baada ya kuanza kampeni za urais za Donald Trump.
Kwa mujibu wa ripoti, kulikuwa na makundi 34 yaliyo dhidi ya Waislamu Marekani mwaka 2015 lakini makundi hayo yaliongezeka na kufika 101 mwaka 2016.
Uchunguzi umebaini kuwa matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu ya Trump wakati akigombea urais ndicho chanzo kikuu cha kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu Marekani.
Uchunguzi huo ambao umefanywa na shirika la Southern Poverty Law Centre umebaini kuwa, mwaka 2016 ulivunja rekodi Marekani kwa kiwango cha chuki dhidi ya Waislamu.
Shirika hilo limesema kwa ujumla kuna makundi zaidi ya 900 yenye kueneza chuki dhidi ya wengine kote Markeani. Makundi hayo yanajumuisha pia yale ya wazungu wanazi wenye misimamo mikali ya kibaguzi na pia makundi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao wanataka kujitenga na Marekani kutokana na dhulma wanazotendewa.
Shirika hilo limesema kuibuka Trump ghafla mwaka 2016 katika kampeni za uchaguzi wa rais ni jambo ambalo lilichangia kiasi kikubwa kuongezeka wimbi la makundi ya kibaguzi na yenye chuki ambayo yalikuwa hayajitokezi hadharini kwa miongo mingi katika jamii ya Marekani.
Baada ya ushindi wa Trump na kuapishwa kwake Januari 20 kumeshuhudiwa hujuma dhidi ya misikiti na vituo vya Kiislamu Marekani na pia katika nchi jirani ya Canada.