Mwislamu wa kwanza katika historia ya Marekani kugombea ugavana
Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Marekani, Mwislamu anagombea ugavana wa jimbo la Michigan.
Abdulrahman Mohamed El-Sayed, daktari Mmarekani mwenye asili ya Misri ametangazwa kuwa mgombea wa ugavana wa jimbo la Michigan.
Iwapo atashinda uchaguzi huo, Abdulrahman Mohamed atakuwa gavana wa kwanza Mwislamu na kijana zaidi nchini Marekani. Daktari huyo ambaye amezaliwa katika jimbo hilohilo la Michigan ana umri wa miaka 32.
Abdulrahman Mohamed ambaye anasifika sana kwa kufanya marekebisho katika wizara ya afya ya Detroit amesema imani na maadili yake ya kidini yamekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio hayo kama mtumishi wa umma. Amesisitiza kuwa itikadi zake za Kiislamu zina umuhimu mkubwa sana kwake.
Jimbo la Michigan ni miongoni mwa majimbo ya Marekani ambako harakati za kuhujumu na kupiga vita Uislamu zimeshika kasi zaidi.
Ripoti zinaonesha kuwa, wimbi la hujuma na mashambulizi dhidi ya Uislamu na Waislamu limeshadidi zaidi nchini Marekani tangu Donald Trump achaguliwe kuwa rais mpya wa nchi hiyo.