Kuongezwa muda vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia
Jumatatu iliyopita Umoja wa Ulaya, ulitangaza kurefusha vikwazo kwa muda wa miezi sita mingine dhidi ya shakhsia na mashirika kadhaa ya Russia na eneo la Crimea, yaani hadi tarehe 15 Septemba mwaka huu.
Kwa utaratibu huo, marufuku ya kusafiri kwa shakhsia 150 wa Russia imerefushwa tena kwa miezi sita zaidi sambamba na mali zao kuendelea kuzuiliwa katika nchi za umoja huo, kutokana na mgogoro uliotokea katika eneo la Crimea hapo mwaka 2014. Vikwazo hivyo vinahusu marufuku ya kuingia Ulaya na kuzuiliwa fedha za shakhsia hao. Vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia vinaweza kuwa na maana ya kuendelea siasa za umoja huo zilizojengeka juu ya msingi wa mashinikizo dhidi ya Moscow.
Ukweli ni kwamba, licha ya kufanyika mashauriano na mazungumzo ya mara kadhaa baina ya Brussels na Moscow kwa ajili ya kutatuliwa tofauti zilizopo, lakini Umoja wa Ulaya bado umeendelea kushikilia msimamo wake kwa ajili ya kuanza upya mahusiano ya kiuchumi na kibiashara na Russia. Hii ikiwa na maana ya umoja huo kusisitizia pendekezo lake la kutaka kukabidhiwa upya eneo la Crimea kwa Ukraine sambamba na kubadilika siasa za sasa za Moscow kuhusiana na mgogoro wa eneo la mashariki mwa Ukraine. Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na waitifaki wake wa Magharibi hususan Marekani, inaituhumu Russia kwamba inachochea machafuko nchini Ukraine, katika hali ambayo Moscow imekuwa ikikanusha kuhusika kwa aina yoyote na mgogoro huo.
Russia imeshatangaza mara kadhaa kuwa, madamu maslahi na matakwa yake kuhusiana na Ukraine yataendelea kupuuzwa na serikali ya Kiev yenye mielekeo ya Kimagharibi na pia na Umoja wa Ulaya na Marekani, basi haitokuwa tayari kubadilisha siasa zake kuhusiana na suala zima la Ukraine. Wakati huo huo Russia haikufumbia macho hatua za madola ya Magharibi dhidi yake, ambapo katika hatua mbadala hadi sasa imeyawekea vikwazo mashirika kadhaa ya umoja huo na Marekani. Kwa kuzingatia kuwa, kabla ya kuibuka mgogoro wa Ukraine, Umoja wa Ulaya ulihesabiwa kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Russia, hivyo vikwazo vya Moscow dhidi ya umoja huo vimeyasababishia madhara makubwa mashirika makubwa ya EU.
Suala hilo limekuwa likipewa mazingatio na viongozi wa Russia na katika fremu hiyo, siku chache zilizopita, Dmitry Medvedev Waziri Mkuu wa nchi hiyo alifichua hasara ya kiasi cha dola bilioni 100 iliyozipata nchi Magharibi kutokana na vikwazo vya nchi hizo dhidi ya Moscow. Suala hilo ndilo lililoibua tofauti ndani ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya juu ya ima kusitishwa au kuendelezwa vikwazo dhidi ya Russia. Katika hali hiyo kuna mitazamo miwili ndani ya Umoja wa Ulaya. Kwanza ni wa nchi zenye mahusiano ya karibu sana na Marekani, ambazo zinataka kuendelezwa vikwazo dhidi ya Russia hadi pale Warussia watakaposalimu amri mbele ya matakwa ya Magharibi kuhusiana na kadhia nzima ya Ukraine. Nchi zilizoko kwenye mrengo huo ni Uingereza ambayo inahesabiwa kuwa mshirika mkubwa wa kistratijia wa Washington.
Nchi za Mashariki mwa Ulaya hususan nchi tatu za eneo la Baltic, yaani Poland, Jamhuri ya Watu wa Czech na Slovakia, nazo zinafuata mrengo huo, yaani kutokana na ugomvi wa muda mrefu uliopo baina yao na Moscow, zinapendelea kuendelezwa vikwazo hivyo dhidi ya Russia. Kinyume na mrengo huo, ni nchi za Umoja wa Ulaya ambazo kabla ya kutokea mgogoro wa Ukraine, zilikuwa na mahusiano mapana ya kibiashara na kiuchumi na Russia, ambapo kutokana na kupunguzwa au kukatwa mahusiano hayo, zimekumbwa na hasara kubwa ya kifedha na kiuchumi. Sasa nchi hizo zinataka kupunguzwa au kuondolewa kabisa vikwazo dhidi ya Russia. Katika uwanja huo nchi hizo ni pamoja na Ugiriki, Hungary, Cyprus, Slovenia, Croatia na Uhispania, ambazo zinataka kuangaliwa upya siasa za sasa kuihusu Russia.
Pamoja na hayo hata baadhi ya nchi kama vile Ujerumani ambayo hapo awali ilipendekeza kuondolewa kwa hatua vikwazo dhidi ya Russia, hivi karibuni imetangaza wazi kuwa, madamu Moscow haitotekeleza makubaliano ya Minsk, yaliyofikiwa katika mji mkuu wa Belarus, yanayohusu utatuzi wa mgogoro wa eneo la mashariki mwa Ukraine, basi haitokuwa tayari kuunga mkono hatua yoyote ya kutaka kuondolewa vikwazo hivyo. Suala hilo linaashiria kuwa, licha ya serikali mpya ya Marekani kutaka kuboresha uhusiano wake na Moscow, lakini nchi za Umoja wa Ulaya zimeendelea kushikilia msimamo wao dhidi ya taifa hilo.