Waislamu walaani marufuku ya Hijabu katika mahakama ya EU
Waislamu barani Ulaya wamelaani vikali hatua ya Mahakama ya Uadilifu ya Ulaya kutoa hukumu kuwa waajiri wanaweza kuwazuia wafanyakazi wa kike Waislamu kuvaa hijabu kazini.
Nchini Ujerumani, Baraza Kuu la Waislamu limekosoa vikali hukumu hiyo likisema inakiuka haki za kimsingi ambazo zimeainishwa katika mikataba muhimu ya Ulaya kuhusu haki za binadamu.
Naye Bekir Altas, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Milli Gorus, inayowakutanisha pamoja Waislamu wenye asili ya Uturuki huko Ujerumani, amelaani hukumu ya mahakama hiyo.
Mahakama ya Haki ya Ulaya (ECJ) yenye makao yake huko Luxembourg Jumanne iliyopita ilipasisha marufuku ya vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu.
Kwa mujibu wa hukumu ya mahakama hiyo, waajiri wa Ulaya wanaweza kuwazuia wafanyakazi wao kuvaa nembo za kidini likiwemo vazi staha la hijabu.
Hii ni hukumu ya kwanza kutolewa na mahakama ya Ulaya kuhusu mjadala wa vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika maeneo ya kazi.
Waislamu Ulaya wanasema, hatua hii si tu kwamba ni ubaguzi wa wazi dhidi ya wanawake wa Kiislamu, bali pia imewapa mamlaka makubwa waajiri kutumia hukumu hiyo kwa ajili ya kuwabana zaidi wafanyakazi wa kike Waislamu na kuwapa hiari ya ama kuvua mavazi yao ya hijabu au kufutwa kazi.