Marekani: Chaguo la kuishambulia kijeshi Korea Kaskazini lipo mezani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26536-marekani_chaguo_la_kuishambulia_kijeshi_korea_kaskazini_lipo_mezani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema Washington haitavumilia tena chokochoko za Korea Kaskazini na ikibidi, US itashambulia kijeshi Pyongyang.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 18, 2017 07:18 UTC
  • Marekani: Chaguo la kuishambulia kijeshi Korea Kaskazini lipo mezani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema Washington haitavumilia tena chokochoko za Korea Kaskazini na ikibidi, US itashambulia kijeshi Pyongyang.

Rex Tillerson, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani aliyasema hayo jana Ijumaa akiwa Korea Kusini, katika ziara ya nchi kadhaa za Asia na kubainisha kuwa, chaguo la kuivamia kijeshi Korea Kaskazini lipo mezani.

Tillerso alisema: "Wacha niweke wazi suala hili, sera ya uvumilivu wa kistratejia imekwisha. Tunatathmini hatua mpya za kiusalama na za kidiplomasia dhidi ya Korea Kaskazini."

Wanajeshi na silaha za Korea Kaskazini

Waziri wa Mambo ye Nje wa Marekani ambaye leo anatazamiwa kuitembelea China ameongeza kuwa, iwapo Pyongyang itanyanyua mpango wake wa silaha kwa kiwango ambacho tutahisi ni tishio, hatutakua na budi kugeukia chaguo la kijeshi.

Mapema mwezi huu, Washington ilisema kuwa imeanza kutuma nchini Korea Kusini mfumo wa ulinzi wa makombora wa THAAD, baada ya Korea Kaskazini kusema kuwa, jaribio lake la hivi karibuni la makombora ni maandalizi kwa ajili ya kuzishambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Japan.

Katika mazungumzo ya simu, Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe walisema majaribio haya mapya ya makombora yaliyofanywa na Korea Kaskazini ni vitisho vilivyoingia katika 'hatua mpya'.