Waislamu China marufuku kuwa na ndevu ndefu, niqab
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27158-waislamu_china_marufuku_kuwa_na_ndevu_ndefu_niqab
Serikali ya China imepiga marufuku wanaume Waislamu kufuga ndevu ndefu na wanawake Waislamu kuvaa niqabu katika eneo la Xinjiang lenye Waislamu karibu milioni 10 wa kabila la Uigur.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 01, 2017 23:36 UTC
  • Waislamu China marufuku kuwa na ndevu ndefu, niqab

Serikali ya China imepiga marufuku wanaume Waislamu kufuga ndevu ndefu na wanawake Waislamu kuvaa niqabu katika eneo la Xinjiang lenye Waislamu karibu milioni 10 wa kabila la Uigur.

Sheria hizo mpya zimeanza kutekelezwa Jumamosi ambapo pia Waislamu wamewekewa vizingiti kadhaa  kama vile kuzuiwa harusi za kidini na marufuku ya watoto kusomea nyumbani. Aidha ni marufuku kuwapa watoto majina ambayo yanadaiwa kuonyesha ukereketwa wa kidini.

China imedai kuwa sheria hizo mpya zinalenga kukabiliana na kile kinachodaiwa kuwa ni misimamo mikali ya kidini lakini watetezi wa haki za binadamu wanasema vizingiti hivyo ni ukandamizaji wa haki za Waislamu.

Waislamu wa kabila la Uigur nchini China

Mwaka jana Serikali ya China, kwa mara nyingine, iliwaamuru wanafunzi, wafanya kazi wa umma na hata wakaazi wa kawaida katika eneo la Xinjiang kutofunga Saum ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mwezi Machi, Rais Xi Jinpinga wa China alitoa wito kwa jeshi la nchi hiyo kuweka 'Ukuta Mkubwa wa Chuma' katika eneo hilo lenye Waislamu wengi. Watetezi wa haki za binadamu wanasema sera kandamizi za China zimepelekea kuwepo hali ya taharuki katika eneo la Xinjiang ambapo katika miaka yahivi karibuni kumeripotiwa mapigano baina ya jeshi na wenyeji mara kadhaa ambapo mamia wameuawa.