10 wauawa katika mripuko wa Metro nchini Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27238-10_wauawa_katika_mripuko_wa_metro_nchini_russia
Maafisa usalama wa Russia wametangaza kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika mripuko uliotokea ndani ya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Saint Petersburg wamefikia watu 10 na wengine watano wamejeruhiwa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 03, 2017 10:43 UTC
  • 10 wauawa katika mripuko wa Metro nchini Russia

Maafisa usalama wa Russia wametangaza kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika mripuko uliotokea ndani ya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Saint Petersburg wamefikia watu 10 na wengine watano wamejeruhiwa.

Shirika la habari la TASS la Russia limewanukuu maafisa usalama wa nchi hiyo wakisema kuwa, vituo saba vya Metro vya mji wa Saint Petersburg vimefungwa baada ya kutokea mripuko huo leo Jumatatu. Maafisa wa usalama wa mji wa Saint Petersburg wamelifunga eneo la kuingilia kwenye vituo hivyo na kuna uchunguzi mkubwa unafanyika katika maeneo hayo.

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema baada ya tukio hilo kwamba maafisa usalama wa nchi hiyo wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina wa kubaini iwapo tukio hilo ni la kigaidi au ni ajali.

Rais Vladimir Putin wa Russia

 

Maafisa wa Metro wa Moscow, mji mkuu wa Russia nao wamesema kwamba, wameimarisha ulinzi katika njia za treni za chini ya ardhi mjini humo kwa mujibu wa sheria za kiusalama za usafiri na uchukuzi za Russia.

Kwa muda sasa magenge ya kigaidi yamekuwa yakitoa taarifa na vitisho kwa njia ya sauti yakitishia kufanya mashambulizi ya kigaidi nchini Russia. Moscow kwa kushirikiana na jeshi la Syria imetoa pigo kubwa sana kwa magaidi nchini Syria na imeamua kuweka ulinzi mkali katika miji mbalimbali ya Russia kama tahadhari ya kujilinda na mashambulizi ya kigaidi.

Hadi hivi sasa makumi ya magaidi waliorejea kutoka Syria au raia wa nchi za kigeni hasa za Asia ya Kati wametiwa mbaroni katika miji mbalimbali ya Russia ikiwemo Moscow wakiwa na vifaa vya kutengeneza mabomu au mabomu yaliyokusudiwa kutegwa katika maeneo yenye watu wengi huko Russia.