UNESCO yakosoa sera za Israel za kukalia kwa mabavu Palestina
(last modified Wed, 03 May 2017 11:40:19 GMT )
May 03, 2017 11:40 UTC
  • UNESCO yakosoa sera za Israel za kukalia kwa mabavu Palestina

Kamati ya Utendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Utamaduni na Sayansi UNESCO Jumanne ilipitisha azimio ambalo liliulaani utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kukiuka sheria za kimataifa katika mji wa Quds (Jerusalem) na Ukanda wa Ghaza.

Azimio hilo aidha liliutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uheshimu utambulisho wa kihistoria wa mji wa Quds.

Azimio hilo la UNESCO limetaja Israel kuwa "utawala ghasibu' na limeutaka usitishe uchimbaji wake usio na kikomo na utengenezaji wa njia za chini kwa chini na miradi mingine  katika eneo la Mashariki mwa Quds Tukufu.

Azimio hilo limetolewa ikiwa inakaribia mwaka wa 69 wa kuundwa utawala bandia wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina na Quds Tukufu, kibla cha kwanza cha Waislamu.

Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel amekasirishwa mno na upasishwaji wa azimio hilo dhidi ya Israel. Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amedai kuwa azimio lililopasishwa na UNESCO ni  la udiplomasia wa kipuuzi.

Mwaka jana pia UNESCO ilipitisha azimio jingine ambalo lilitilia shaka uhusiano wa Uyahudi na maeneo matakatifu ya Quds jambo ambalo liliughadhibisha sana utawala wa Kizayuni. Kufuatia azimio hilo, utawala wa Kizayuni ulisimamisha kwa muda uhusiano wake na UNESCO.

Hadi sasa UNESCO imepitisha maazimio kadhaa dhidi ya utawala huo wa Kizayuni na kuutaja kuwa utawala ghasibu ambao unapaswa kutekeleza maamuzi ya kimataifa na maazimio ya UNESCO kuhusu turathi za kihistoria za Quds Tukufu eneo ambalo mwaka 1981 lilitembuliwa na UNESCO kama mojawapo ya turathi za dunia.

Kamati ya Utendaji ya UNESCO Aprili mwaka 2015 pia iIiushurutisha utawala ghasibu wa Israel uwazuie Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada na wanajeshi wa Israel kuuvamia na kuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa na Wapalestina.

Aidha UNESCO pia iliutaka utawala wa Israel usitishe mpango wa kubadilisha majengo ya Msikiti wa Al Aqsa kutumiwa na bunge la utawala huo, Knesset. Hali kadhalika UNESCO iliutaka utawala huo usitishe mpango wa kuyapa majina ya Kiyahudi maeneo ya kale na barabara za mji wa Quds. Lakini utawala huo wa Kizayuni umepuuza kabisa maazimio hayo ya UNESCO na taasisi zingine za Umoja wa Mataifa na kuendeleza sera zake za kuuharibu mji wa Quds sambamba na kufuta utambulisho wake wa kihistoria, kitaifa na kidini.

Hatua za utawala wa Kizayuni katika Msikiti wa Al Aqsa ni ukiukwaji wa wazi wa maazimio ya kimataifa ikiwani ni pamoja na azimio la mwaka 1954 la The Hague kuhusu 'Kulinda maeneo ya kiutamaduni katika vita na mapigano."

Hatua za Israel Quds pia ni ukiukwaji wa azimio la 1972 kuhusu kulindwa turathi za kiutamaduni na kimaumbile. Hayo yote yanaashiria namna utawala wa Kizayuni wa Israel unavyokiuka sheria na mikataba ya kimataifa. Kuhusiana na hili, katika miaka ya hivi karibuni na kufuatia uungaji mkono wa walimwengu kwa watu wa Palestina, tumeona UNESCO  na taasisi zingine za kimataifa zikivunja kimya chao na kutoa maazimio ya kuwaunga mkono watu wa Palestina.

Ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina

Kujiunga Palestina na UNESCO na kupandishwa bendera yake katika taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Paris mwaka 2011 ni kati ya hatua zilizochukuliwa na UNESCO kwa ajili ya kuunga mkono haki za watu wa Palestina.

Misimamo ya mara kwa mara ya UNESCO katika kuulani hatua haribifu za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Quds Tukufu ni jambo linalotokana na walimengu kuipa umuhimu kadhia ya Palestina sambamba na kuulani utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa hakika ujumbe wa UNESCO ni kuwa hatua za Israel hazina uhalali wowote na hivyo walimwengu wanapaswa kutafakari kuhusu hatua za kivitendo zinazopaswa kuchukuliwa kusitisha jinai za utawala huo ghasibu.

Hatua ya utawala wa Israel ya kuituhumu UNESCO na taasisi zingine za kimataifa ni jambo litakaloufichua zaidi utawala huo katika uga wa kimataifa na kuweka wazi utambulisho wake wa kukiuka sheria za kimataifa sambamba na kuupelekea kutengwa zaidi duniani.